Afrika Kusini huenda ikajiondoa kwenye ICC

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Afrika Kusini huenda ikajiondoa kwenye ICC

Afrika Kusini imesema kuwa huenda ikajiondoa kutoka kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC yenye makao yake makuu huko Hague Uholanzi kufuatia jaribio la kumkamata rais wa Sudan Omar al Bashir alipokuwa nchini humo majuzi.

Hata hivyo Nusra akamatwe kufuatia agizo la mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita dhidi yake kutokana na mashtaka ya mauaji ya kimbari.

Lakini baada ya kikao maalum cha baraza la mawaziri nchini humo, serikali ilitoa onyo kuwa huenda ikalazimika kujiondoa kutoka kwa makubaliano yeyote na mahakama ya ICC kutokana na sababu kadha.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais huyo wa Sudan alikuwa nchini Afrika Kusini kwa mkutano wa viongozi wa bara Afrika

''Serikali inawajibu wake wa kimataifa lakini pia inawajibu wake kisiasa''taarifa hiyo ilisema.

''iwapo hatutakuwa na suluhisho maalum itakayotusaidia kutanzua taharuki iliyopo kwa sasa nafikiri serikali yetu haitakuwa na budi ila kujiondoa kutokana na makubaliano yeyote na ICC''iliendelea kusema.

Mahakama ya Afrika Kusini ilikuwa imemuagiza rais Bashir kusalia nchini humo huku ikijadiliana kuhusu iwapo agizo hilo la kukamatwa kwake litekelezwe au la.

Lakini kabla ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wake rais Bashir aliondoka nchini Afrika Kusini na kurejea nyumbani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Bashir alipokewa kwa shangwe na nderemo aliporejea Khartoum

Rais huyo wa Sudan alikuwa nchini Afrika Kusini kwa mkutano wa viongozi wa bara Afrika na kwamba serikali ilikuwa inajua kwamba ilihitajika kumkamata kwa kuwa ni mwanachama wa ICC.

Kwenye taarifa yake , ICC ilisema kuwa waranti mbili za kumkamata Bashir bado zipo.

Rais al Bashir anatafutwa na mahakama ya uhalifu wa kivita kuhusiana na uhalifu ulitokea katika jimbo la Darfur na anakabiliwa na kesi inayohusiana na uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki.