Carlos Tevez amerejea Boca Juniors

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Carlos Tevez amerejea Boca Juniors

Mshambulizi wa Argentina na washindi wapili katika kombe la mabingwa mwaka huu Juventus Carlos Tevez amerejea katika klabu yake ya zamani ya Boca Juniors.

Tevez, 31, alianzia huko huko Argentina katika Boca Juniors kabla ya kuondoka mwaka wa 2004 kwa ziara iliyomweka barani ulaya kwa kipindi cha miaka 9.

Tevez ambaye alitamba Uingereza katika vilabu vya Manchester United, Manchester City na West Ham kabla ya kuhamia Italia kujiunga na mabingwa msimu huu Juventus .

Tevez alifunga mabao 20 katika ligi kuu ya Serie A.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Tevez aliisaidia Argentina kuilaza Colombia katika robo fainali ya Copa America

Kulikuwa na uvumi wake kurejea Uingereza katika dirisha la uhamisho katika msimu wa joto ambapo jina lake lilihusishwa na uhamisho kwenda Liverpool, Atletico Madrid ama Paris St-Germain.

Hatma yake huko Italia ilikuwa imeshabainika baada ya Juventus kusajili huduma za mshambulizi wa Atletico Mario Mandzukic.

Boca Juniors walithibitisha uhamisho huo licha ya kuwa Tevez alikuwa akipasha joto benchi katika robo fainali ya Copa America Argentina ilipokuwa ikikabiliana na Colombia.

Ilikuwa sadfa kwani punde tu baada ya Boca kutangaza uhamisho huo,Tevez aliingia uwanjani kama mchezaji wa akiba na akafunga penalti iliyoiwezesha Argentina kufuzu kwa nusu fainali ya Copa America.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Tevez, alishinda mataji mawili ya ligi nchini Uingereza na mawili nchini Italia.

Rais wa Boca,Daniel Angelici alisema''ni siku njema sana kuwa Carlos Tevez anarejea nyumbani,nina hakika kuwa ataimarisha ushindani wetu katika klabu ya Boca.

Tevez, alishinda mataji mawili ya ligi nchini Uingereza na mawili nchini Italia.

Alifunga mabao 38 katika mechi 110 alipoichezea Boca mara ya kwanza.

Wakati huo aliisaidia kutwaa taji la ligi kuu mwaka wa 2003 mbali na kutawazwa mchezaji bora katika ligi hiyo ya Marekani ya kusini kwa miaka mitatu mfululizo.