Ugiriki yaomba miaka 2 kunusuru uchumi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu nchini Ugiriki wakipanga misururu kuchukua fedha katika mashine za kutolea fedha

Serikali ya Ugiriki imeomba makubaliano mapya na nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya euro ili kunusuru uchumi wake, ikiwa imebakiwa na saa chache kabla ya kulipa deni la euro bilioni 1.6 (£1.1bn) linalodaiwa na Shirika la Fedha Duniani, IMF.

Ugiriki imeomba mkataba mpya wa msaada wa euro bilioni 29.1 wa miaka miwili kupitia mpango wa kunusuru uchumi wa nchi za euro.

Mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya euro wamejadili ombi la Ugiriki kupitia mkutano wao kwa njia ya mawasiliano ya video uliofanyika Jumanne jioni, lakini hawakuweza kutoa uamuzi.

Iwapo Ugiriki itashindwa kulipa deni la IMF, nchi hiyo itakuwa hatarini kuondoka katika umoja wa nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya euro.

Tume ya Ulaya, ambayo ni moja ya wakopeshaji wa Ugiriki, inataka nchi hiyo kukusanya kodi na kupunguza matumizi.

Hakuna nchi iliyoendelea kiuchumi ikashindwa kulipa deni la IMF.

Huku kukiwa na wasiwasi kwa Ugiriki kushindwa kulipa deni lake kubwa la euro bilioni 323 na uwezekano wa kutoka katika umoja wa nchi zinazotumia sarafu ya euro - misururu mirefu ya watu inaendelea katika mashine za kutolea fedha nchini Ugiriki, ambapo kiwango cha juu kinachoruhusiwa kutolewa kwa siku ni euro 60.