Ugiriki yaomba miaka 2 kuikomboa uchumi

Alexis Tsipras Waziri Mkuu wa Ugiriki Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bw Tsipras amepinga vikali masharti ya wakopeshaji wa nchi yake

Ugiriki imeomba mwafaka wa miaka miwili wa kujikomboa kiuchumi kutokana na madeni inayodaiwa na jumuiya ya Ulaya.

Mapendekezo yake yanajumuisha kufanya marekebisho mengi yatakayoiwezesha nchi hiyo kulipa madeni yake.

Tangazo hilo limetolewa karibu dakika za mwisho.

Mapema Ugiriki ilikuwa imethibitisha kuwa itashindwa kulipa deni lake kufikia mwisho wa siku (Juni 30).

Wanahabari wanatilia shaka mapendekezo haya ya Anthens.

Chanzela wa Ujerumani Angela Merkel alinukuliwa akisema mapema kuwa hakutazamia matokeo haya.

Mapema leo, Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras aliwaomba wapiga kura wakatae masharti ya wakopeshaji wa nchi hiyo wakati wa kura ya maoni hapo Jumapili.

Bw Tsipras amesema kuwa Ugiriki itaweza kushauriana zaidi na kupata suluhu la mzozo wa sasa wa kifedha.

Siku ya mwisho kwa Ugiriki kugharamia madeni yake ni Jumanne wiki hii (Juni 30) ambapo inatakiwa kulipa deni la Euro bilioni 1.6, kwa shirika la fedha duniani (IMF).

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Viongozi wa Eu wameonya huenda Ugiriki ikaondoka kanda ya sarafu ya Euro

Viongozi wa muungano wa Ulaya wameonya hatua ya kukataa kulipa madeni yake ni sawa na Ugiriki kujiondoa kutoka kwenye muungano wa mataifa yanayotumia sarafu ya Euro.

Hata hivyo Waziri Mkuu Tsipras amesema hataki nchi yake kuitema Euro.

Mazungumzo kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake yalivunjika wiki jana, hatua iliyosababisha benki za nchi hiyo kufungwa.