Ugiriki yaonywa kuhusu kura ya 'La'

Raia wa Ugiriki Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Raia wamegawanyika huku wengi wakianza kuhamia kambi ya 'Ndio'

Ugiriki imeonywa dhidi ya kupiga kura ya 'La' wakati wa kura ya maoni hapo Jumapili kwa sababu haitasaidia kutatua matatizo ya kiuchumi yanayokumba taifa hilo.

Hii ni kwa mujibu wa kiongozi wa mawaziri wa fedha kutoka kanda inayotumia sarafu ya Euro.

Bw Jeroen Dijsselbloem amesema haya baada ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Minister Alexis Tsipras kuwaomba raia wake kupiga 'La' akisema itasaidia nchi hiyo kuafikiana na wakopeshaji wake.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kumekua na milolongo mirefu kwenye benki Ugiriki wateja wakitoa fedha zao

Wakati huo huo kwa siku ya pili mfululizo, milolongo mirefu imeendelea kuhushudiwa katika benki nchini Ugiriki.

Bw Dijsselbloem, ambaye ni Waziri wa fedha wa Uholanzi amesema kura ya 'La' itafanya vigumu kwa pande zote kuafikiana.

Benki za Ugiriki zilifungwa wiki hii baada ya Benki kuu ya Ulaya kukataa kutoa mkopo wa dharura kwa Ugiriki.

Vyombo vya habari vimesema biashara nyingi zimesitisha shughuli zake kwa hofu ya kukosa fedha huku waajiri wengi wakiwapa waajiriwa wao likizo za mapema.

Raia wa Ugiriki wamegawanyika huku kura ya maoni ya karibuni ikionyesha wengi wameanza kujiunga na upande wa 'Ndio'.