Matimbo yenye Mauti pwani ya Kenya

Image caption Matimbo yenye Mauti pwani ya Kenya

Watu saba wanaaminika kufa kutokana na maporomoko ya matimbo yaliyoko Pwani ya Kenya katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Wengine wakibomolewa viungo na baruti zilizoachwa kwenye matimbo hayo.

Mwandishi wetu Ferdinand Omondi aliwatembelea baadhi ya waathiriwa na kupata hadithi za matimbo ya vifo.

Ni saa ya maakuli katika eneo la Mabatani, Kaunti ya Kwale, huko Kenya.

Mama Mwanaidi Athman anabarizi nje ya nyumba yake iliyo hatua chache karibu na timbo la Mchangarawe, akiwa amejifunika na hijab ya samawati, na uso uliojaa uchungu.

Anawatazama wanafunzi wakielea nyumbani kutoka shuleni.

Wawili kati yao wangekuwa wake lakini hawako tena.

Walikufa kwenye ajali ya timbo la Mchangarawe lililoko hatua chache tu kutoka boma lake.

Mwanaidi anasema vijana watano walienda kuoga kwenye maji yaliokusanyika timboni, wakati ukuta wa timbo ulipoporomoka na kuwaangukia.

“Tuliaanza kufukua ilikuwatafuta watoto, tukasukumana , tukampata mtoto wa mwenzangu ambaye alikuwa amefunikiwa kidogo amepona.''

Image caption Watu saba wanaaminika kufa kutokana na maporomoko ya matimbo yaliyoko Pwani ya Kenya

''Akaanza kufukua tena, tukampata Ismaili ambaye ni mwanangu ashakufa.''

''Tukafukua tena tukampata kassim ambaye ni wa mwenzangu ashakufa.''

Watoto wanne walikufa hiyo siku.

Mwanaharusi Rashid pia alimpoteza mwanaye.

Anaungana na Mwanaidi, na pamoja wanakubali kunipeleka palipotokea ajali.

Lakini wafikapo timboni, uchungu wa mwana unawafanya wanazongwa na mawazo na huzuni wanaanza kulia.

Wakalia kwa uchungu sana. Anapotulia, Bi Mwanaharusi asema timbo hilo lamkera kila siku,

‘’Mimi kwa ufupi sehemu hii nikitembea nalia na nafsi.

''Nikitoka sehemu iko open naona kila kitu.''

Akili yangu iko pale naona watoto wanaanza kutolewa.

''Nafsi inaungua, sina uzima saa hii.’’Kisha anaanza kulia tena

Mchanga katika eneo hili bado ni mwepesi sana, na nikisimama inanipa taswira ya jinsi ilvyokuwa rahisi kwa mchanga huu kuporomoka na kuwaua watoto.

Matimbo kama haya Katika eneo la pwani na maeneo ya mapato madogo kwa wale ambao huja hapa kuvuna.

Lakini kwa wazazi waliopoteza watoto wao, matimbo haya sasa ni kumbukumbu ya mauti, ya jinsi walivyopoteza watoto wao.

Zaidi ya kilomita themanini kutoka hapa, kwenye eneo la Kilifi, kijana mmoja alinusurika kifo, lakini amelemazwa.

Hassan hufunika kichwa chake na shuka, kukinga majeraha ya mdomo wake kutokana na nzi.

Kulingana na baba yake, Majimbo Karisa, mwanaye wa miaka kumi na nne aliokota waya na chuma kwenye timbo moja iliyo karibu, akitarajia kuwa zingemsaidia kuunganisha redio iliyo nyumbani.

‘’Alipunganisha zile waya, akajaribu kutest na mdomo, kwa sababu zile battery hakuwa na uhakika zina moto.

Basi alipogusa tu ile waya na kinywa chake, ile chuma ikamlipukia kwa sababu ilikuwa ni baruti ambayo haijatumika’’, asema Majimbo.

Anameza kila kitu kwa kutumia sindano, Aidha kusema pia imekuwa shida, Shule haendi tena.

Karisa asema mwanawe anahitaji usaidizi mkubwa hadi imembidi baaka kuacha kazi yake ya matimboni kumshughulikia.

‘’Familia bado tunanganga kupata nafasi ya kumpeleka hospitali, lakini hali ni ile ya shida shida….

Na mimi siwezi kumwacha maana hali ya shida ni lazima iwe niko karibu naye, kuanzia matatizo ya maumivu, hata malaji pia, niwe niko karibu kwa sababu kuongea hawezi. ‘’

Ongezeko la idadi ya watu wanaokufa na kuumia kwa sababu ya matimbo sasa inaleta wasiwasi katika eneo la Pwani ya Kenya.

Image caption Sheria za sasa zimeweka faini za kutowajibika ya dola thelathini tu

Kuna zaidi ya matimbo ishirini zinazofanya kazi huku maswala yakiibuka kuhusu kudhibitiwa kwao.

Shirika lisilo la kiserikali la Human Rights Agenda, limerekodi vifo saba kwa miezi miwili.

Mtetezi wa Haki Yusuf Lule asema hali hii inatokana na sheria duni pamoja na utekelezaji hafifu na serikali za kitaifa na za kaunti.

Na ingawa kunayo sheria nyingine zinaoongoza kama uchimbaji wa Mchangarawe, sheria hizi hazifuatwi.’’

Sheria za sasa zimeweka faini za kutowajibika ya dola thelathini tu, huku anayesababishwa kifo timboni akitakiwa kulipa dola mia mbili kama faini.

Katika kaunti ya Kwale ambapo watoto wane waliaga, sheria za uchimbaji zinarekebishwa, lakini waziri wa Madini Abdalla Mwafimbo anasema sheri hizo zitazingatia mapato pia.

‘’Hizi timbo, ingawaje zinaharibu mazingira, na ni tishio kwa wananchi, pia ni mapato kwa wananchi wenyewe.

Image caption Familia zikiomboleza wapendwa wao waliozama timboni

Huko Kilifi, Majimbo Karisa ana matumaini kuwa siku moja atakusanya pesa za kutosha kumpeleka mwanawe kupata upasuaji wa kumrejeshea mdomo.

Huko Kwale timbo lilifunikwa lakini wazazi wangali wanahofia usalama wa wanao ambao hucheza kwenye matimbo mengine yaliyoko mitaani.

Bila sheria kabambe za kuwadhibiti wenye matimbo na kuwalipa fidia waaathirika, usalama wa wengi bado uko hatarini.