Kura kwa bendera ya kikaburu Marekani

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bendera hiyo imehusishwa na enzi za utumwa

Wabunge katika jimbo la South Carolina Marekani, wamewasilisha marekebisho mengi kwa sheria hiyo katika bunge la waakilishi wakitaka yajadiliwe leo.

Mmoja wa wabunge hao amesema kuwa kuondolewa kwa bendera hiyo katika majengo ya serikali kutamomonyoa utamaduni na historia ya miaka mingi ya jimbo hilo.

Wanao unga mkono kuondolewa kwa bendera hiyo wameihusisha na karne ya utumwa na ubaguzi wa rangi.

Mswada huo wa kuharamisha bendera hiyo uliwasilishwa baada ya mwanamume mmoja kuwaua kwa kuwapiga risasi waumini tisa wa kikristu weusi katika kanisa moja la asili ya Kiafrika nchini humo.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Maandamano ya kupinga kuondolewa kwa bendera hiyo

Alionekana kupiga picha akiwa na bendera hiyo.

Bunge la seneti lililo na wengi kutoka upande wa Republican lilipitisha mswada huo kwa kura thelathini na sita dhidi ya kura tatu.

Wakati huo huo, kamishna wa polisi katika mji wa Baltimore Marekani, Anthony Batts amefutwa kazi, kufuatia kuongezeka kwa visa vya uhalifu.

Hii inafuatia ghasia zilizozuka Aprili baada ya kijana mmoja mweusi Freddie Gray, kuuawa akiwa mikononi mwa polisi.

Meya wa jiji hilo Stephanie Rawlings-Blake, amesema kuwa malalamiko ya kila mara dhidi ya kamishna huyo wa polisi yanahujumu marekebisho yoyote kufanywa katika idara hiyo ya polisi na watu kuendelea na maisha yao.

Amesema kuwa ongezeko la mauaji katika siku za hivi punde linamaana kuwa mabadiliko yanahitajika katika uongozi wa idara hiyo ya polisi. Maafisa sita wa polisi wamefunguliwa mashtaka kuhusiana na kifo cha Freddie Gray.