Wazazi wamtumia mwana wao kama 'chambo'

Haki miliki ya picha afp
Image caption Wanaharakati nchini India wamekuwa wakipinga ubakaji nchini humo

Maafisa wa polisi kusini wa jimbo la Kerala nchini India wamemkamata mama na baba wa kambo wa msichana mmoja kwa madai ya kumlazimisha kufanya biashara ya ngono kwa kipindi cha miaka miwili.

Msichana huyo wa umri wa miaka 13 ameokolewa na kupelekwa katika nyumba moja inayosimamiwa na serikali.

Aliwaambia washauri wake kwamba wazazi wake huwatafuta wateja na kumlazimisha kufanya tendo la ngono nao.

Mamaake alikiambia chombo kimoja cha habari kwamba huwatoza wateja hao kati ya dola 47.

Image caption Baadhi ya washukiwa waliokamatwa

Maafisa wa polisi wanasema kuwa wamewatambua wateja 25 kati ya 40 ambao walilipa ili kulala na msichana huyo.

Kumi wengine akiwemo wakala wameshtakiwa kwa kuhusika katika kesi hiyo.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 37 ana watoto saba mkubwa akiwa na miaka 24 na mdogo akiwa na miaka minne.

Mumewe mwenye umri wa miaka 55 alifanya kazi kama dereva na huwatafuta wateja kwa kuonyesha picha ya msichana huyo kulingana na maafisa wa polisi.

Familia hiyo inaishi katika nyumba ya kukodi katika mji wa Kottakal wilayani Malappuram kaskazini mwa jimbo hilo.