Siasa zapamba moto ndani ya CCM Tanzania

Moto wawaka chama tawala CCM Tanzania
Maelezo ya picha,

Moto wawaka chama tawala CCM Tanzania

Chama tawala nchini Tanzania Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea na mikutano yake ya mwaka.

Alasiri hii halmashauri kuu ya chama hicho inafanya kikao chake kupata majina matatu, halafu baadae leo jioni mkutano mkuu wa chama hicho unatarajiwa kukaa kupigia kura jina moja kati ya hayo matatu.

Yule atakayeibuka mshindi kati ya watatu hao ndiye atakaye kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu

Hata hivyo kutangazwa kwa majina matano na kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa (CC-NEC) ya chama hicho jana usiku, kuliibua mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo, ambapo watatu wa wajumbe 32 wa kamati hiyo waliibuka wazi na kupinga uteuzi wa majina hayo mbele ya vyombo vya habari

Maelezo ya picha,

Watanzania kumjua ni nani atakayekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao

Wajumbe waliopinga uteuzi huo ni Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa

Wajumbe hao walidai kuwa kanuni za utendaji katika vikao vilivyotangulia kamati kuu zimekiukwa na kufafanua kwamba kamati hiyo ilipokea majina matano kutoka kamati ya maadili na usala, badala ya kupewa majina yote ya walioomba kuteuliwa, halafu yenyewe ndiyo ichambue majina matano.

“Kanuni zinasema Kamati Kuu itapokea majina ya waombaji wote na ikishafanya uchambuzi wa kila muombaji, yakiwemo maoni ya kamati ya usalama na maadili, ndiyo huchagua majina matano yanayofikishwa mbele ya Halmashauri Kuu,” alihoji Dk. Nchimbi

Maelezo ya picha,

Mpasuko huu unaonekana kuwa mwanzo wa kutimia kwa utabiri wa wachambuzi mbalimbali

Mpasuko huu unaonekana kuwa mwanzo wa kutimia kwa utabiri wa wachambuzi mbalimbali ambao walionya mchakato huu unahatarisha uhai wa chama kikongwe nchini Tanzania

Majina matano yaliyopitishwa na Kamati Kuu ni Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. John Magufuli (Waziri wa Ujenzi) Dk. Asha-Rose Migiro (Waziri wa Katiba na Sheria) January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia) na Balozi Amina Salum Ali (Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Tume ya Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Marekani)

Kufikia Jumapili, tarehe 12. Julai, Watanzania watakuwa wamejua ni nani atakayekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM kwa uchaguzi mkuu ujao