Viongozi wa Ulaya kuamua hatima ya Ugiriki

Image caption Waziri wa uchumi wa Ugiriki awasili Brussels

Siku muhimu ya majadiliano kuhusu madeni ya Ugiriki, imeanza mjini Brussels, kuamua iwapo Ugiriki itabaki katika umoja wa nchi zinazotumia sarafu ya euro au la.

Jopokazi, linachambua ombi la Ugiriki, kutaka msaada mpya kabla ya mawaziri wa fedha kukutana.

Serikali ya Ugiriki inapendekeza kuchukua hatua kali zaidi za kubana matumizi, kama kuzidisha kodi ya mapato na kuzidisha umri wa kuweza kustaafu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mkutano wa kujadili madeni ya Ugiriki, mjini Brussels, utaamua iwapo Ugiriki itabaki katika umoja wa nchi zinazotumia sarafu ya euro au la

Serikali inatumai hatua hizo zitaweza kuipatia mkopo wa dola bilioni-60, na kusamehewa baadhi ya mikopo ya sasa.

Mapendekezo hayo yalikubaliwa kwa sauti kubwa katika bunge la Ugiriki, kwenye kikao cha jana usiku.

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya, wanatarajiwa kujadili mapendekezo hayo ya Ugiriki siku ya jumapili.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bunge la Ugiriki liliunga mkono kwa asilimia kubwa mapendekezo la hivi punde la serikali ya waziri mkuu Alexis Tsipras

Awali, Bunge la Ugiriki liliunga mkono kwa asilimia kubwa mapendekezo ya hivi punde la serikali ya waziri mkuu Alexis Tsipras yenye lengo la kumaliza tatizo la deni la nchi hiyo.

Baada ya kikao kilichoendeleka hadi usiku wabunge 252 waliipa serikali idhini ya kufanya mazungumzo na wakopeshaji wake.

Waziri mkuu Alexis Tsipras alishindwa kupata kura za wabunge kumi kutoka chama chake cha Syriza wakiwemo mawaziri wawili wa serikali na spika wa bunge.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waziri wa zamani wa fedha Yanis Varoufakis hakuhudhuria kikao hicho.

Waziri wa zamani wa fedha Yanis Varoufakis hakuhudhuria kikao hicho.

Bwana Tsipras alikiri kuwa mabadiliko yaliyopendekezwa yalikuwa nje ya ahadi zilizotolewa na chama chake.

Mapendekezo hayo yatajadiliwa na mawaziri wa fedha wa nchi za ulaya hii leo na pia viongozi wa ulaya kesho jumapili.