Mexico:Milioni 4 kutambua aliko 'shorty'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mexico imetoa dola milioni 4 kutambua aliko 'shorty'

Serikali nchini Mexico imetangaza kiangaza macho cha dola milioni 4 kwa yeyote ambaye atasaidia kukamatwa kwa mfanyibiashara mkubwa zaidi wa madawa ya kulevya ambaye alitoroka kutoka jela lenye ulinzi mkali huko Mexico.

Shughuli kubwa ya kumtafuta Joaquin Guzman ambaye pia anajulikana kama ''Shorty'' alitoroka gerezani akipitia njia ya chini kwa chini .

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari waziri wa masuala ya ndani alisema kuwa maafisa katika gezera hilo ni lazima walimsaidia Guzman kutoroka.

Aliongezea kusema kuwa endapo itathibitishwa kuwa ukweli alisaidiwa na maafisa wa idara ya Magereza basi hicho kitakuwa ni kitendo cha uhaini.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Njia ya chini kwa chini aliyotumia mfanyibiashara wa mihadarati kutoroka gerezani

Maafisa watatu wa vyeo vya juu wa gereza hilo akiwemo mkurugenzi wa gereza wamefutwa kazi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Mexico ameitisha mkutano wa magavana wa majimbo ili kujadili namna ya kuepusha vurugu zinazoweza kutokea kufuatia kutoroka kwa mtuhumiwa maarufu wa biashara ya dawa za kulevya.

Vyombo vya usalama ndani ya Mexico na maeneo ya jirani kwa sasa vina msaka Joaquin Guzman anayedaiwa kuwa ni mfanyabiashara nguli wa dawa za kulevya anadaiwa kutoroka katika mazingira yanayodaiwa kuwa ni ya rushwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa wa kulinda usalam wameshika doria nje ya gereza la Altiplano

Naye Rais wa Mexco, Enrique Pena Nieto, anasema kuwa ana Imani kuwa idara za usalama zitamkamata mtuhumiwa huyo anayedaiwa kuwa mhimili duniani kwa biashara hiyo ya dawa za kulevya na ambaye alitoroka kutoka kati kati ya ulinzi mkali.

Hata hivyo Rais Pena Nieto amesisitiza kuwa uchunguzi wa kina unatakiwa kufanywa kubaini aliko Joaquin Guzman.