Afrika yaomboleza Mzee Ojwang

Image caption Gazeti la Daily Nation lilitangaza kuaga dunia kwa Mzee Ojwang

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameliongoza taifa kumuomboleza kifo cha muigizaji stadi wa kipindi maarufu cha televisheni ''Vitimbi'' aliyeaga dunia jana usiku katika hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta mjini Nairobi.

Katika risala zake Rais Kenyatta alimmiminia sifa kochokocho mwendazake Benson Wanjau ambaye amekuwa maarufu katika runinga ya Kenya kwa miaka mingi.

Mzee Ojwang hatari alitawala ulingo wa uigizaji katika vipindi vya runinga ya taifa KBC vya Vitimbi, Vioja Mahakami, Vituko na Kinyonga.

Maelfu ya mashabiki wake kutoka Kenya na Tanzania walimkumbuka kwa vichekesho vyake vilivyowaongoa kwa miaka mingi.

Image caption Jonathan Ondieki akiomboleza katika mtandao wa Twitter

Edward Senkondo kutoka Tanzania ameandika katika mtandao wa faceboook

Image caption Risala kutoka kwa aliyekuwa makamu wa rais wa Kenya

''Poleni sana Kenya na familia ya sanaa ya maigizo. Alikua muigizaji mzuri sn na mchekeshaji mahili sana.

Mungu amlaze pema peponi amina''.

Zilahenda Mgozi Mzungu vilevile kutoka Dar es Salaam Tanzania

''Poleni sana wakenya na africa nzima huyu mzee alikuwa akinivutia sana ktk uigizaji wake MUNGU ampumzishe kwa amani''

Aidha magezeti yote makuu nchini Kenya yalimlimbikizia sifa kedekede gwiji huyo anayetajwa kama baba ya uigizaji nchini humo.

Gazeti la Star lilipachika picha yake chini ya mada ''Mzee Ojwang mhakiki wa serikali ya kenya ametuacha''

Gazeti la Daily Nation lilitangaza kifo cha muigizaji huyo nguli aliyekuwa na miaka 78.

Image caption Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema runinga haitakuwa kama ilivyokuwa katika enzi zake muigizaji stadi wa ''Vitimbi'' Mzee Ojwang

Ojwang aliaga dunia baada ya madaktari kushindwa kutibu kuenea kwa kichomi(nimonia)

Hata hivyo kinachobainika ni kuwa vigogo wengi wa usanii haswa nchini Kenya huishi maisha ya kifahari wakiwa katika kilele cha talanta zao ila wanapostaafu huishia kuishi maisha ya ufukara mwingi.

Miezi kadha iliyopita wasanii wenza waliogiza na Mzee Ojwang wakiongozwa na 'mke wake'' Mama Kayai walilazimika kuchanga fedha ilikumpeleka muigizaji huyo hospitalini baada ya kugundua kuwa alikuwa amepofuka.

Kwa sasa mipango ya mazishi imeanza kufanyika nyumbani kwake.

Image caption Gazeti la Star kutoka Kenya lilichapisha risala ya rais katika mtandao wa Twitter

Ojwang amemuacha nyuma mjane Augusta Wanjiru ambaye walijaaliwa naye watoto wawili Patricia Njeri na Michael Karira.

Japo walikuwa wachumba katika kipindi cha Vitimbi, mama Kayai (Mary Khavere) wawili hao walikuwa marafiki tu maishani.