Rais Mseveni na usuluhishi wa Burundi

Image caption Raia wa Burundi wakipiga kura

Rais wa Uganda Yoweri Museveni leo ameingia siku yake ya pili ya mazungumzo ya amani nchini Burundi.

Ikiwa imebaki siku chache tu kufanyika kwa uchaguzi wa Rais, inaonekana kuna nafasi ndogo ya Rais Museveni kuweza kushawishi lolote kuhusiana na msimamo wa Serikali ya Burundi kuhusiana na uchaguzi wa Burundi.

Mara baada ya kuwasili nchini Burundi kwa njia ya barabara akitokea Uganda, Rais Museven amewaambia wanasiasa wa Burundi, makundi ya kijamii na kidini kwamba Burundi kama ilivyo mataifa mengine ina matatizo ambayo yanatafsiriwa kama matokeo ya fikra tofauti ndani ya vichwa vya watu

Museveni amewakumbusha raia wa Burundi moja ya jambo baya lililowahi kutokea nchini humo na ambalo halipaswi kuwepo kwa sasa ambalo ni mgawanyiko wa kikabila kati ya Wahutu na Watusi, na jambo la pili ni kudhani kuwa madarakani ndilo jambo la mhimu kuliko mambo mengine yote yanayoweza kuleta ustawi wa taifa zima

Katibu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Richard Sezibera amesema kuwa uchaguzi mkuu wa Burundi,haupaswi kusababisha raia kuikimbia nchi yao na kwenda kutafuta hifadhi nchi jirani

Jana Usiku Rais Mseveni amekuwa na majadiliano ya pamoja na viongozi wa kambi ya upinzani wa Burundi,mashirika ya kiraia na uwakilishi wa viongozi wa Kidini.

Rais Museveni leo atakutana na kundi jingine la wawakilishi wa serikali na viongozi wengine wastaafu katika mazungumzo