Yemen:Maafisa wa serikali wawasili Aden

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Uwanja wa ndege wa mji wa Aden

Mawaziri kadhaa na maafisa wa ngazi za juu wa upelelezi wa serikali ya Yemen iliyoko uhamishoni wanasemekana kutua katika mji wa Aden ulioko kusini mwa nchi hiyo.

Duru kutoka kwa shirika la habari la Reuters zasema kuwa walifika mjini humo kwa helikopta, katika ziara hiyo ya kwanza baada ya vita vikali vilivyodumu miezi mitatu sasa.

Wamekuwa wakiishi uhamishoni nchini Saudi Arabia tangu rais Abd-Rabbu Mansour Hadi, alipolazimika kukimbia Yemen mwezi Machi mwaka huu baada ya serikali ya Iran kuwapa ufadhili wa kijeshi wanamgambo wa Houthi.

Wapiganaji wenye silaha wanaoungwa mkono na Saudi Arabia katika harakati za mashambulizi ya angani, wamewafurusha wanamgambo wa Houthi kutoka mji huo wa Aden.