Messi azindua uwanja wa Gabon2017

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Messi azindua uwanja wa kombe la mataifa ya Afrika 2017 Gabon

Mshindi wa tuzo la mchezaji bora duniani mara nne ,Lionel Messi, amekutana na rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba.

Mchezaji wa Argentina na mabingwa wa ligi kuu ya Ulaya Barcelona aliweka jiwe la msingi la uwanja utakaotumika kuandaa mechi za fainali za kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2017.

Mchezaji huyo maarufu wa kilabu cha Barcelona ,mshindi wa tuzo la Mfalme wa Uhispania Copa del Rey na ligi ya Ulaya msimu uliopita,alizindua rasmi mchakato wa ujenzi katika uwanja wa soka wa Port-Gentil.

Sherehe za uzinduzi huo zilifanyika kwenye eneo kubwa la mchanga ambapo uwanja huo wa soka utajengwa.

Ni ziara ya kwanza ya mshambuliaji huyo wa Argentina nchini Gabon na aliweka saini yake kwenye jezi zinazovaliwa na mashabiki wake , kabla ya kuweka jiwe la msingi akiambatana na rais.

Image caption Uwanja huo mpya utakua na uwezo wa kuwapokea mashabiki 20,000

" Nilipokua Barcelona miaka michache iliyopita , nilikutana na Messi ambaye aliniambia kwamba atakuja kunitembelea mjini Libreville," alisema rais wa Gabon.

" Ni ahadi aliyonipa.''

''Ni mtu anayetimiza ahadi ."

Uwanja huo mpya utakua na uwezo wa kuwapokea mashabiki 20,000 na unatarajiwa kuandaa mechi kuanzia mwezi Novemba 2016 katika michezo ya awali ya shindano hilo.