Habre: Kesi imeahirishwa hadi Septemba

Haki miliki ya picha
Image caption Rais wa zamani wa Chad arejeshwa kortini

Kesi ya kihistoria dhidi ya Kiongozi wa zamani wa Chad Hissene Habre iliyokuwa imerejeshwa mahakamani leo nchini Senegal sasa imeahirishwa hadi mwezi Septemba.

Mahakama imetoa muda huo kwa wakili wapya wa kiongozi huyo wa zamani wa kimla kujiandaa kwa kesi inayomkabili ya makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili na uhalifu wa kivita .

Bwana Habre ambaye amekataa kuitambua mahakama hiyo alikataa kuzungumza mahakamani huku akiwashauri wakili wake wasimwakilishe mahakamani.

Hatua hiyo ilimlazimu hakimu kuingilia kati na kushurutisha apewe mawakili wapya.

Haki miliki ya picha
Image caption Jana aliondolewa kizimbani huku wananchi wakimfokea.

Hapo ndipo alipoagiza mahakama hiyo iahirishe vikao vyake hadi mwezi septemba kuwaruhusu mawakili hao wapya kujiandaa kikamilifu kuambatana na sheria.

Kesi hiyo mjini Dakar iliahirishwa hapo jana baada ya wafuasi wa rais huyo wa zamani kuzua kihoja mahakamani wakiidunisha mahakama hiyo naye Bwana Habré, alikataa kutambua uhalali wa mahakama hiyo..

Aliondolewa kizimbani huku wananchi wakimfokea.

Hakimu aliamuru arejeshwe tena leo kizimbani ilikukutana na baadhi ya watu aliosemekana kuwatesa.

Haki miliki ya picha
Image caption Bwana Habre anakanusha shutuma hizo.

Kesi hiyo ya kihistoria ni ya kwanza ya aina yake ambapo nchi moja ya Afrika imemshitaki kiongozi wa zamani wa taifa jingine.

Bwana Habre anashutumiwa kwa kuhusika na vitendo vya ukatili na mauaji ya maelfu ya watu wakati wa enzi ya utawala wake kuanzia 1982 hadi 1990.

Bwana Habre anakanusha shutuma hizo.

Magazeti nchini Senegal yameandika ripoti kuu kutokana na matukio ya jana mahakamani.

Aidha mengine yanashauri rais wa sasa Idriss Deby naye afikishwe mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya bosi wake wa zamani.

Kesi hiyo inafuatia miaka 25 ya kampeni za kumfikisha mbele ya sheria.

Haki miliki ya picha
Image caption Rais Habre aliongoza Chad kuanzia 1982 hadi 1990.

Wengi miongoni mwa watu wanaodaiwa kuwa waathirika wa uhalifu uliotekelezwa na Bwana Habre, wamekua wakitoa wito wa kufunguliwa mashtaka dhidi yake tangu alipopinduliwa mamlakani na kukimbilia uhamisho nchini Senegal mwaka wa 1990.

Mnamo mwaka 2005 mahakama ya Ubelgiji ilitoa kibali cha kumkamata, ikidai kuwa na haki ya kimataifa ya kufanya hivyo.

Hata hivyo baada ya mazungumzo na Umoja wa Afrika AU, muungano huo uliiomba serikali ya Senegal kuendesha kesi dhidi Habre " kwa niaba ya Afrika ".