Nkurunziza ajivunia kuleta demokrasia

Haki miliki ya picha
Image caption Raia wa Burundi wapiga kura

Raia wa Burundi wanapiga kura leo katika uchaguzi wa rais uliojaa utata, miezi kadhaa baada ya jaribio lililokwama la mapinduzi.

Burundi imeshuhudia maandamano na machafuko tangu rais anayemaliza muda wake Perre Nkurunziza kutangaza anawania tena awamu ya tatu madarakani.

Mwandishi wa BBC Salim Kikeke anaarifu kuwa Rais Nkurunziza aliwasili katika kituo cha kupigia kura akiendesha baiskeli, huku akiwa katika ulinzi mkali.

Alishangiliwa na kundi la wanawake katika mji wake wa kuzaliwa wa Ngozi, wakati akielekea kupiga kura.

Ajivunia Demokrasia

Akizungumza kwa ufupi baada ya kupiga kura, Nkurunziza amesema baada ya miaka mingi wa uimara wa kisiasa, Burundi sasa inaelekea katika mwelekeo ulio sawa upande wa demokrasia, kwa kuwapa wananchi uhuru kuchagua wanayemtaka kuwa rais.

Hata hivyo wagombea wa nafasi hiyo ya Urais kupitia vyama vya upinzani nchini humo, wamegomea uchaguzi wakisema kwamba Nkurunziza hana haki ya kugombea tena.

Milio ya risasiburundi na magruneti imesikika katika mji mkuu wa nchi hiyo Bujumbura, huku watu wawili wakiarifiwa kuuawa, usiku wa kuamkia leo.