Kura zaendelea kuhesabiwa, Burundi

Image caption Kura zahesabiwa Burundi

Nchini Burundi kura zinaendelea kuhesabiwa, kufuatia uchaguzi wenye utata uliofanyika jana.

Maafisa wa Tume ya Uchaguzi nchini humo wanasema watu wengi wamejitokeza katika maeneo mengi vijijini, huku watu wachache wakijitokeza katika baadhi ya maeneo mijini.

Katika kitongoji kimoja mjini Bujumbura masanduku yaliyokuwa na kura zilizohesabiwa yalikuwa yakikusanywa. Maafisa wa uchaguzi nchini humo wameiambia BBC, idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura mjini ni ndogo sawa na asilimia kati ya 29 na 30 na kwamba kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa alikuwa akiongoza. Anasema idadi ndogo ya watu iliyojitokeza kupiga kura inaweza kusababishwa na mashambulizi ya risasi na magruneti yaliyokuwa yakirindima siku ya mkesha wa uchaguzi.

Masanduku ya kura na matokeo ya uchaguzi huo nchi nzima yanapaswa kupelekwa katika ofisi za Tume ya Uchaguzi katika siku chache zijazo.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, matokeo ya jumla yanaweza kutangazwa Ijumaa.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, UNHCR maelfu ya watu wameikimbia nchi hiyo.

Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa walitaka uchaguzi huo kuahirishwa, kwa kusema kuwa mazingira hayaruhusu uchaguzi ulio huru na wa haki.

Upinzani nchini humo wanapinga Rais Pierre Nkurunziza kuwania nafasi ya tatu.