Obama:Utalii nchini Kenya kufaidika

Image caption Obama:Utalii nchini Kenya kufaidika

Sekta ya Utalii nchini Kenya imeanza kupata afueni baada ya Uingereza kuondoa vikwazo vyake dhidi ya raia wake kuzuru nchi hiyo.

Hata hivyo, wadau wa utalii wanasema wageni kutoka ulaya wameanza kunesha nia yao ya kurejea katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Aidha kuna matumaini kuwa ziara ya rais wa Marekani Barack Obama nchini Humo pia itachangia ufufuo wa Utalii ambao ulikuwa umedorora kwa kiasi kikubwa kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Image caption Dalili za kufufuka kwa sekta hiyo zinaonekana.

Lakini shirika linalopigania utalii wa Pwani nchini Kenya hautarajii mabadiliko mara moja.

Mwandishi wetu Ferdinand Omondi alizungumza na mwenyekiti wa Shirika hilo Mohammed Hersi huko Mombasa.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa zaidi ya watu elfu ishirini walipoteza kazi zao kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyopelekea mataifa ya magharibi kutoa ilani dhidi ya watalii kuzuru Kenya.

Lakini sasa dalili za kufufuka kwa sekta hiyo zinaonekana.

Wageni kutoka ulaya sasa wameanza kuulizia gharama za vyumba vya kulala mbali na kuuliza iwapo hali ya usalama imeimarika.

Haki miliki ya picha
Image caption Duka la Westgate ambamo watu 67 waliuawa na wanamgambo wa Al Shabab

Hersi pia amesema kuwa kuja kwa Rais Barrack Obama wa Marekani kutapiga jeki sifa ya Kenya kiusalama, lakini hatarajii waMarekani kufurika Kenya eti kwa sababu rais wao amefika.

Watu 67 waliuawa wakati wa makabiliano ya siku nne wakati wanamgambo wa Al Shabab na maafisa wa Usalama kufuatia shambulizi la kigaidi katika maduka ya Westgate.

Duka hilo lilifunguliwa wiki moja iliyopita .

Wachanganuzi wanasema kuwa kufunguliwa kwa maduka hayo kabla ya ziara ya rais wa Marekani Barack Obama ni ishara ya imani kwa usalama wa Kenya.

Kundi hilo la kiislamu limetekeleza mashambulizi mengine mabaya nchini Kenya tangu litokee shambulizi la Westgate likiwemo lile la chuo kikuu cha Garissa ambapo watu 150 waliuawa.