Solar yanufaisha wanawake Unguja

Image caption Wanawake wa Unguja wajifunza kuwa wataalam katika nyanja ya sayansi

Hali ya uchumi na mfumo wa maisha umeanza kubadilika kwa baadhi ya wakazi wa Matemwe, kaskazini mwa Unguja, nchini Tanzania.

Hii ni baada ya kuanzishwa kwa mradi ujulikanao kama Barefoot Solar ambao unalenga wanawake wenye umri mkubwa ambao wanaopewa mafunzo ya ufundi wa kutengeza taa zinazotumia nishati ya jua na hatimae kuziuza kwa wana kijiji wenzao kwa bei nafuu.

Kuwepo kwa bidhaa hiyo, kumewafanya wakazi hao kuachana na matumizi ya taa zinazotumia mafuta ya taa ambazo, licha ya kuwa na gharama, lakini pia ni hatari kwa maisha ya watu.

Image caption Mwakilishi wa maswala ya Wanawake Umoja wa Mataifa nchini Tanzania,Anna Collins-Falk

"Kwa kweli tunawalenga kina mama wenye umri mkubwa, ambao wanaelimishwa na kupewa mafunzo nchini India. Hawa ni wanawake wa vijijini ambao baadhi yao hawajui kusoma wala kuandika, wamekwenda nchini India, katika chuo cha mafunzo ya solar cha Barefoot. Wamepewa mafunzo ya uhandisi wa solar, na baada ya kurudi, wao wenyewe wamekuwa wahandisi wa mambo ya solar, na wanasambaza taa zinazotumia nishati hiyo kijijini mwao," amefafanua Anna Collins-Falk ambae ni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Kitengo cha Wanawake nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Fatma Athman ambae ni mmoja wa wahandisi wa solar, anaelezea jinsi matumizi ya nishati ya jua yalivyobadilisha maisha katika nyumba yake.

Image caption mitambo ya solar ikipata nishati ya jua

"Nyumbani tulikuwa tukitumia vibatali na mafuta ya taa. Lakini tangu niliporudi kutoka India kusoma, tumebadilika sana, kwa sababu hatutumii tena vitabali, na badala yake tunatumia taa za solar," Fatma Athumani alimwelezea mwandishi wa BBC Aboubakar Famau pindi alipowatembelea katika chuo hicho cha ufundi wa mambo ya solar kilichopo kaskazini mwa Unguja.

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, mfumo dume bado umeelezwa kuwa ni changamoto katika jamii. Mwanshamba Hamisi Makame mwenye umri wa miaka 50 anasema wanaume mara nyingi huwacheka na kuwashangaa jinsi wanavyowaona wakipanda juu ya nyumba kwa ajili ya kufunga vifaa vinavyotumia nishati ya jua.

Wengi wa wanawake hawa walikuwa wakijishughulisha katika miradi mbalimbali ikiwemo ukulima bila mafanikio yoyote. Hivyo mradi huu wa Barefoot Solar unaodhaminiwa na Umoja wa Mataifa, serikali ya Tanzania na ile ya India umetoa fursa ya kuwepo kwa njia mbadala ya kujipatia kipato na kuheshimika katika jamii.