IOC yaonya wanariadha wanaotumia madawa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais wa IOC,Thomas Bach amesema IOC haitamhurumia mwanariadha yeyote aliyeshinda nishani ya dunia kupitia njia isiyo halali.

Rais wa kamati ya Olimpiki duniani, Thomas Bach amesema kuwa, IOC haitamhurumia mwanariadha yeyote aliyeshinda nishani ya dunia kupitia njia isiyo halali.

Bach alikuwa akiyasema hayo punde baada ya kupokea taarifa inayoonesha kashfa ya matumizi ya dawa za kuusisimua misuli katika riadha.

Akiongea katika mkutano mkuu wa IOC huko Kuala Lumpur, rais huyo wa IOC anasema kuwa anasubiri matokeo ya kina kufuatia uchunguzi wa shirika linalodhibiti matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu- WADA.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Thuluthi moja ya wanariadha wametumia madawa ya kuongeza nguvu mwilini

Ripoti ya vyombo vya habari kutoka Ujerumani na Uingereza zinasema kuwa asilimia tatu ya washindi wa medali katika mashindano makubwa ya riadha kati ya mwaka 2001 na 2012 zilinyakuliwa na wanariadha ambao damu zao zinashukiwa kuwa na chembechembe za dawa hizo haramu.

Mkurugenzi mkuu wa zamani wa WADA Dick Pound, ameonya kuwa kutakuwa na mzozo mkubwa mno miongoni mwa wanariadha iwapo hilo litathibitishwa.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mkenya Rita Jeptoo aliyepigwa marufuku kwa kutumia madawa ya kuongeza nguvu mwilini

Uchunguzi ulioendeshwa na gazeti la Uingereza la Sunday Times na kituo cha habari cha Ujerumani cha ARD, baada ya taarifa zilizovuja za maelfu ya matokeo ya uchunguzi wa damu kutoka kwa shirikisho hilo kuonesha kuwa mashrikisho ya riadha hayajakuwa yakiwajibika ipasavyo na mengine haswa yakificha ukweli.

Shirikisho la riadha duniani IAAF imetetea jitihada zake za kupambana na matumizi ya madawa ya kusisimua misuli kwa kuongeza idadi na ubora wa vifaa vinavyotumika kupima matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini.