Wahamiaji 300 wafikishwa Italia

Haki miliki ya picha msf
Image caption Vikosi vya waokoaji wakiwa katika operesheni ya kuwaokoa wahamiaji baada ya Boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka

Zaidi ya watu 300 waliookolewa baada ya boti kupinduka karibu na ufuo wa Libya siku ya jumatano wamewasili nchini Italia.walifikishwa katika bandari ya Palermo kwa meli ya jeshi la wanamaji wa Ireland ,ambacho kilikuwachombo cha kwanza kufika katika eneo la tukio.

Meli ya Jeshi la wanamaji la Ireland liliwasili Alhamisi jioni likiwa na manusura 367 ndani yake, kati yao wanawake 13 na watoto 12. Shirika la madaktari wasio na mipaka Medicin sans frontiers pia wameiambia BBC kuwa pia kulikuwa na miili takriban 25 iliyoopolewa.

Kwa mujibu wa msemaji wa Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR, Barbara Molinario, Watu waliookolewa wanatoka nchini Syria,Bangladesh, Eritrea na wengine kadhaa kutoka nchi za Afrika kusini mwa jangwa la sahara.

Manusura hao wanapatiwa huduma za msingi kama vile chakula,maji,mavazi,na huduma za afya, wengine wengi wanapewa ushauri nasaha na huduma za saikolojia baada ya kufikwa masaibu.

Hivi sasa wamepelekwa katika vituo mbalimbali nchini Italia ambapo watakuwa kwenye vituo hivyo kwa siku kadhaa kabla ya kuanza utaratibu kwa kuomba hifadhi nchini humo.

Inakisiwa kuwa kulikuwa na watu 600 kwenye Boti hiyo, idadi ambayo hata hivyo ni vigumu kuthibitisha, hivyo hakuna anayefahamu idadi ya watu ambao hawajapatikana mpaka sasa.

Wahamiaji takriban 2000 wamepoteza maisha mwaka huu pekee wakati wakijaribu kusafiri kupitia bahari ya maditerrania wakielekea Ulaya.