Aliyeua watu 12 anusurika hukumu ya kifo

Haki miliki ya picha AP
Image caption Aliyeua watu12 anusurika hukumu ya kifo

Mtu aliyewaua watu 12 katika maonyesho ya filamu moja katika eneo la Colorado nchini Marekani katika mji wa Denver miaka mitatu iliyopita amehukumiwa kifungo cha maisha lakini akanusurika kifo kwa sababu washauri wa mahakama hawakukubaliana kwa kauli moja iwapo anyongwe kwa makosa yake au la.

James Holmes, mwenye umri wa miaka 27 alipatikana na hatia ya kuwaua watu 12 na kuwajeruhi wengine 70.

Wakili wake alidai kuwa mteja wo alikuwa mwenda wazimu wakati wa tukio hilo.

Washauri wa mahakama hiyo walikubaliana kuwa japo alikuwa na matatizo ya kiakili, Holmes,anastahili kuchukua lawama kwa mauaji aliyoyatekeleza.

Hata hivyo jopo hilo lilitofautia iwapo kweli atawajibikia makosa yake basi anyongwe ama afungwe maisha.

Kulingana na kanuni za sheria za Marekani, jopo la washauri likishindwa kuafikiana kwa kinywa kimoja, mahakama inampa mtuhumiwa kifungo cha maisha jela bila fursa ya kusamehewa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption James Holmes, mwenye umri wa miaka 27 alipatikana na hatia ya kuwaua watu 12 na kuwajeruhi wengine 70

Mmoja wa washauri alinukuliwa na runinga ya NBC akisema kuwa 'wengi wa washauri walikubali kuwa alikuwa na matatizo ya kiakili alipotekeleza mauaji hayo japo asilimia kubwa vilevile ikipinga kuwa anastahili kupewa adhabu ya kifo'.

'Kwa hivyo tukashindwa kutoa hukumu'

Jopo hilo lilijumuisha wanawake 9 na wanaume 3 lilijulishwa mahakamani na jaji Carlos Samour katika mji wa wa Centennial ijumaa iliyopita.

Mamake Holmes bi Arlene alibubujikwa na machozi ya furaha hukumu hiyo ilipotolewa mahakamani.

Shirika la habari la AFP liliripoti kuwa ''bi Arlene aliegemea mumewe na akaanza kububujikwa na machozi''

Hata hivyo kwa wale walionusurika kufuatia shambulizi hilo miaka mitatu iliyopita ilikuwa ni huzuni na hasira.

Haki miliki ya picha AP
Image caption George Brauchler , alinukuliwa akisema ''nahisi alistahili kupewa adhabu ya kifo'

Bi Ashley Moser, ambaye alilemazwa na Holmes na pia akapoteza mwanawe wa kike mwenye umri wa miaka 6 katika shambulizi hilo alitikisa kichwa chake kwa uchungu na akaegemea kiti cha magurudumu cha mhanga mwenza ambaye naye alipoozwa kufwatia shambulizi hilo.

Kiongozi wa mashtaka wa serikali bwana George Brauchler , alinukuliwa akisema

''nahisi alistahili kupewa adhabu ya kifo'

'Aliua angestahili naye kufa.'

'Lakini mahakama imeamua ilivyotaka na hivyo hatuna budi ila kukubali kauli ya mahakama.''