Shambulizi la Kigaidi Mali limezimwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu 8 wauawa na magaidi Mali

Maafisa wa kikosi maalum cha kupambana na magaidi wa Mali wamevamia hoteli iliyokuwa imetekwa na washambuliaji wa kigaidi hapo jana.

Uvamizi huo wa asubuhi na mapema katika mji wa Sevare uliwaokoa mateka kadhaa wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Lakini idadi kamili ya waliokolewa na uraia wao haujulikani kufikia sasa.

Msemaji wa Polisi wa Mali alisema kuwa maiti za watu watano wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Waislamu wenye itikadi kali ilipatikana ndani ya yoteli hiyo ya Byblos.

Jumla ya watu 13 wamefariki tangu watu wenye bunduki kushambulia hoteli hiyo katikati mwa jiji la Sevare wakiwa kwenye pikipiki.

Wakishambulia kambi ya wanahewa kabla ya kuteka hoteli hiyo.

Hadi sasa haijulikani na kundi gani hasa lililoteka hoteli hiyo.

Siku za hivi majuzi wapiganaji wa Kiislamu wenye itikadi kali wamedai kuhusika na mashambulizi ya hivi majuzi Kusini na katikati mwa Mali.

Hoteli hiyo hutumiwa kwa wingi na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini humo wanaojulikana kama MINUSA.

Image caption Maafisa wa usalama wanaendelea na operesheni ya kudhibiti uslama katika mji huo

Kwa masaa kadhaa, raia wa Ukraine, Urusi na Umoja wa Mataifa walikwama katika hoteli hiyo wakati mapigano yakiendelea .

Hata hivyo taarifa za baadaye zilielezea kuwa watu kadhaa, kukiwemo wageni watano waliokolewa na kikosi maalumu cha jeshi la Mali.

Raia mmoja wa Mali alisema kuwa shughuli za kudhibiti hali ya usalama ndani na nje ya hoteli hiyo zingali zinaendelea.