Waziri China atembelea eneo la mlipuko

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu 112 walipoteza maisha kwenye mlipuko mjini Tianjin

Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang amewatembelea waathiriwa wa mlipuko mkubwa uliotokea kwenye ghala la kuhifadhia kemikali mjini Tianjin.

Mfululizo wa milipuko katika eneo hilo siku ya jumatano, uligharimu maisha ya Watu 112.Watu tisini na watano kati yao wafanyakazi wa kikosi cha zima moto hawajulikani walipo.

Waziri Li amekutana na waliojeruhiwa na waliokosa makazi kutokana na milipuko.

Ofisa wa juu wa jeshi amesema mamia ya tani ya kemikali hatari ya aina ya sodium cyanide imetambuliwa katika maeneo mawili ilipotokea milipuko.

Kati ya watu 721 waliojeruhiwa, 25 wako katika hali mbaya, huku 33 wakiwa mahututi.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Ndugu wa kikosi cha uokoaji

Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mlipuko.

Ndugu za waliopotea na wakazi wa eneo lililoathirika walifanya maandamano kadhaa wakieleza hasira yao.

Wamedai kuwa hawajapata taarifa za kutosha kutoka kwa Serikali kuhusu aina gani ya kemikali zilizo katika ghala hiyo.

Wakati huo huo mitandao kadhaa imefungwa ikidaiwa kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa kuhusu milipuko hiyo.

Shirika la Habari la China, Xhinua limesema mitandao 50 imedaiwa kusababisha hofu kwa kusambaza tetesi.