Goodluck Jonathan ziarani Kenya

Haki miliki ya picha Daily Nation
Image caption Goodluck Jonathan ziarani Kenya

Aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan,aliwaacha wakaazi wa eneo la Narok Kusini mwa Kenya vinywa wazi alipotua katika eneo hilo maarufu kwa watalii kwa likizo.

Jonathan alikuwa na familia yake alitua kwa ndege mbili za kibinafsi katika uwanja wa ndege ulioko kwenye mbuga ya wanyama ya Maasai Mara.

Ndege moja ilikuwa imembeba Jonathan na familia yake huku ndege ya pili ikiwa imewabeba maafisa wa usalama wa Kenya wanaompa ulinzi mkali katika ziara yake ya siku tatu katika mbuga hiyo ya kitaifa.

Jonathan ambaye alishindwa katika uchaguzi mkuu na Rais wa sasa jenerali Muhammad Buhari aliandamana na mke wake Patience na watoto wake wawili.

Image caption Mbuga ya Maasai Mara ni maarufu kwa sababu ya wanyama wa porini na haswa kuhama kwa kongoni

Licha ya kuwa aliondoka madarakani Jonathan alipewa ulinzi mkali na serikali ya Kenya.

Ziara ya rais mstaafu Jonathan katika mbuga hiyo ya Maasai Mara inasadifiana na kuhama kwa kongoni kutoka mbuga ya wanyama ya Serengeti kuingia Kenya.

Alipokewa na gavana wa jimbo la Narok Samuel Tunai.

Tunai, alisema kuwa ujio wa rais Jonathan na watalii takriban 500,000 kutachochea kufufuka kwa sekta hiyo mbali na kuthibitisha hadhi ya juu ya mbuga hiyo ya Wanyama.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ziara ya Jonathan, inafuatia ile ya mfalme wa Swaziland, Mswati wa III wiki iliyopita

Ziara ya Jonathan, inafuatia ile ya mfalme wa Swaziland, Mswati wa III, aliyezuru mbuga hiyo ya kifahari majuma mawili yaliyopita.

Yamkini Jonathan anaishi katika hoteli ile ile aliyokaa mfalme Mswati.

Kufuatia ziara ya rais wa Marekani mwezi uliopita Kenya imeanza kuwapokea wageni mashuhuru wanaozitembelea mbuga zake za wanyama na fukwe zake za bahari hindi.