Nigeria yawakumbuka wasichana wa Chibok

Haki miliki ya picha
Image caption Wanaharakati wakiandamana Nigeria

Raia wa Nigeria, wameandamana hii leo kuadhimisha siku mia tano tangu wasichana wa shule ya upili ya Chibok, walipotekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram.

Wasichana 219, walitekwa nyara na wanamgambo hao wakiwa shuleni mwao Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Katika miji mikuu ya Lagos na Abuja, makundi ya wanaume, wanawake na watoto waliandamana wakiwa wamevalia mavazi mekundu, kama njia moja ya kuwakumbuka wasichana hao waliotekwa na Boko Haram.

Waandamanaji hao kisha wakafunga vitambaa vyekundu kwenye barabara walizopitia ili kuhakikisha kuwa hatma ya wasichana hao haijasahaulika.

Haki miliki ya picha
Image caption Wasichana hao wa Chiko waliotekwa Nyara

Serikali ya zamani ya nchi hiyo imeshutumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua za dharura kuwakomboa wasichana hao.

Wanaharakati hao wanailaumu serikali ya rais Goodluck Jonathan kwa kutoamini kuwa wasichana hao walikuwa wametekwa nyara.

Kwa usaidizi kutoka kwa nchi jirani na mamluki kutoka Afrika Kusini, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kusambaratisha kundi hilo la Boko Haram, na katika miezi ya hivi karibuni, mamia ya watu wamekombolewa kutoka kwa kundi hilo, lakini kwa siku mia tano iliyopita hatma ya wasichana hao wa Chibok bado haijulikani.

Image caption Wanaharakati wakiandamana Nigeria