Upinzani Tanzania wazindua kampeni

Image caption Mgombea urais wa Muungano wa upinzani Tanzania Edward Lowassa

Mgombea urais wa Muungano wa upinzani nchini Tanzania unaojulikana UKAWA, Edward Lowassa leo amezindua kampeni zake katika kinyang'anyiro cha kugombea urais wa nchi hiyo.

Maelfu ya wakazi wa mji wa Dar es Salaam walijitokeza maelfu kwa maelfu kumsikiliza mgombea huyo ambaye ameahidi kuweka kipau mbele katika sekta ya elimu na kusema kuwa atafanya elimu kuwa bure kuanzia darasa la kwanza hadi Chuo Kikuu.

Chama tawala Chama cha Mapinduzi CCM kilizindua kampeni zake jumapili iliyopita ambapo Mgombea urais wa chama hicho John Magufuli aliahidi pamoja na mambo mengine kuanzisha mahakama maalum ya kushtaki watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Tanzania mwaka huu ina wagombea 8 wanaowania nafasi ya urais ambapo kati ya hao mmoja ni mwanamke.

Kampeni hizo zitaendelea hadi siku moja kabla ya uchaguzi utakaofanyika tarehe 25 Octoba mwaka huu.