Bashir awasili Uchina kwa ziara rasmi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Sudan Omar al Bashir

Rais wa Uchina Xi Jinping amemlaki Rais wa Sudan Omar al-Bashir anayesakwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kama "rafiki wa zamani wa watu wa Uchina.

Bashir ni mmoja wa viongozi wa mataifa ya kigeni watakaohudhuria maonyesho ya kijeshi siku ya Alhamisi kuadhimisha miaka 70 tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia ingawa viongozi wengi wa mataifa ya Magharibi wamesusia hafla hiyo.

"Wewe ni rafiki wa zamani wa watu wa Uchina," XI alisema baada ya kumsalimia Bashir na maafisa wakuu wa serikali ya Sudan walioandamana naye katika uwanja wa ndege.

Rais Xi, alikariri kuwa Uchina imekuwa kwa muda mrefu mshirika mkubwa wa kibiashara na muwekezaji mkuu katika taifa hilo la Afrika.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi wa Uchina

"China na Sudan ni kama kaka wawili ambao pia ni marafiki na washirika wema," Xi alisema.

"Bw Bashir kuja China ni ishara ushirikiano wetu ni thabiti.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, ilitoa kibali cha kukamatwa kwa Bashir, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu mwaka 2009 na kwa tuhuma za mauaji ya halaiki mwaka 2010, kuhusiana na mzozo unaoendelea katika eneo la Darfur.

Tangu wakati huo amezuru mataifa kadha jirani lakini huwa nadra sana kwa rais Bashir kusafiri mbali ambako anaweza kukabiliwa na hatari ya kukamatwa.

Mara ya mwisho kwa Bashir kuzuru Uchina, taifa lililowekeza zaidi katika sekta ya kawi nchini mwake ilikuwa mwaka 2011.

Mzozo Darfur ulainza mwaka 2003 wakati wapiganaji wa makabila yanayoishi eneo hilo walipoasi dhidi ya serikali ya Khartoum iliyo na Waarabu wengi, wakilalamikia kutengwa.

Haki miliki ya picha z
Image caption Rais wa uchina Jinping

Mapigano hayo yamesababisha watu 300,000 kufariki dunia na milioni 2.5 kufurushwa makwao, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Aidha wanajeshi wa Bashir wametuhumiwa kutekeleza dhuluma dhidi ya raia.

Uchina inasema ina sera ya kutoingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine na kawaida imekuwa ikiunda ushirikiano wa karibu na serikali zinazokosolewa na kutengwa na mataifa ya Magharibi kwa msingi wa miongoni mwa mengine ukiukaji wa haki za binadamu.

Uchina na Sudan zimesaini mikataba miwili hii leo, moja ukijumuisha mkataba wa kukuza ushirikiano wa kufaa mataifa hayo mawili na mkataba mwingine wa kuimarisha ushirikiano katika secta ya teknolojia ya safari za anga.