Sambo Dasuki afikishwa mahakamani Abuja

Image caption Sambo Dasuki

Aliyekuwa mshauri wa kitaifa wa masuala ya ulinzi nchini Nigeria, amefikishwa mahakamani mjini Abuja, na kufunguliwa mashtaka ya kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria.

Sambo Dasuki alikuwa mmoja wa maafisa wakuu katika serikali ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan na kwa sasa anafuatiliwa kwa karibu na utawala wa nchi hiyo.

Julai mwaka huu, maafisa wa polisi walinasa shehena ya silaha na risasi nyumbani kwake.

Hata hivyo Dasuku alikana shtaka la kumiliki silaha bila idhini na aliachiliwa kwa dhamana.

Kabla ya rais wa sasa kuchukua uongozi, Dasuki alikuwa mmoja wa maafisa wenye ushawishi mkubwa serikalini na kufikishwa kwake mahakamani ni ishara ya kuwa hatma yake sasa imebadilika.

Yeye ni afisa wa kwanza wa ngazi ya juu katika serikali ya rais Jonathan kufikishwa mahakamani na huenda asiwe wa mwisho.

Haki miliki ya picha Nig Govt
Image caption Rais w a Nigeria Muhammadu Buhari akikagua gwaride la jeshi

Rais Muhammadu Buhari, amebuni tume kadhaa kuchunguza visa vya ufisadi na raia wengi wa Nigeria wanataka kujua jinsi mamilioni ya madola kutoka kwa mauzo ya mafuta ilivyotumika.

Wakati alipokuwa mshauri mkuu wa kitaifa wa ulinzi, Dasuki alikuwa afisa mkuu aliyesimamia operesheni dhidi ya wapiganaji wa Boko Haram.

Mahakama hiyo huenda ikamshurutisha kuelezea jinsi mamilioni ya madola iliyotengewa wizara ya ulinzi ilitumika hasa baada ya kugunduliwa kuwa jeshi la nchi hiyo halikuwa na vifaa vya kisasa kupambana na wanamgambo hao wa Kiislamu.

Lakini baadhi ya raia wa Nigeria wameshutumu rais Buhari kwa kuwafuata wapinzani wake kama njia moja ya kulipisa kisasi.

Miaka 30 iliyopita Sambo Dasuki alikuwa miongoni mwa maafisa wakuu wa jeshi waliohusika na mapinduzi ya serikali yaliyomuondoa madarakani generali Buhari, wakati alipokuwa rais wa nchi hiyo.