Papa Francis alegeza msimamo wa Katoliki

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Papa Francis

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis, ameitikia shinikizo kutoka kwa wanawake wengi waumini wa kanisa hilo na kulegeza msimamo wa kanisa hilo kuhusu uavyaji mimba mwaka ujao wa jubilee.

Huwa ni marufuku kwa waumini wa kanisa Katoliki kuavya mimba, kitendo ambacho huchukuliwa kuwa kosa kubwa katika kanisa hilo.

Papa Francis amesema atawaruhusu mapadri kuwasamehe wanawake wanaoavya mimba na pia madaktari wanaowasaidia kutoa mimba.

Kinyume na watangulizi wake, Papa Francis, huchukulia fadhila na huruma kuwa nguzo kuu zinazozidi nyingine zote.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Waandamanaji nchini Marekani wakitaka serikali kuhalalisha uaviaji mimba

Papa huyo mzaliwa wa Argentina, alisema anafahamu shinikizo ambazo baadhi ya wanawake hukumbana nazo ndipo waavye mimba lakini akasema pia amekutana na wanawake wengi wanaobeba moyoni kovu la alichosema ni uamuzi wa kusikitisha na mchungu.

Ametangaza mwaka wa jubilee, ambao kawaida huhusishwa na msamaha, uadhimishwe na wakatoliki kote duniani kuanzia mwezi Desemba.

Maneno hasa aliyotumia Papa Francis yanaashiria kuwa anafahamu kuna wengi wa wanaojidai kutetea utamaduni wa kanisa hilo ambao hawatafurahishwa na uamuzi wake.

"Nimeamua," Papa Francis alisema. "Bila kujali pingamizi, kuwaruhusu mapadri kutoa msamaha wa dhambi wa kuavya mimba kwa wale wanafanya hivyo na wanaotafuta msamaha wakati wa mwaka wa jubilee."

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Raia wa Ireland wakipinga uaviaji wa mimba