Mwanajeshi wa Uholanzi ajiunga na Islamic state

Image caption Wanajeshi wa Uholanzi nchini Iraq

Mwanajeshi wa jeshi la wanahewa la Uholanzi, anadaiwa kusafiri hadi nchini Syria na kujiunga na kundi la wapiganaji la Islamic State.

Wizara ya ulinzi ya Uholanzi, imesema mwanajeshi huyo ni sajini wa umri mwenye umri wa miaka 26.

Maafisa nchini humo, bado wanaendelea kuchunguza ikiwa kuna mafunzo ya itikadi kali ndani ya jeshi la Uholanzi.

Iwapo tuhuma hizo zitathibitishwa, basi itakuwa mara ya kwanza kwa mwanajeshi anayehudumu katika jeshi la Uholanzi kwenda kujiunga na Islamic State.

Kupitia taarifa wizara ya ulinzi ilisema sajini huyo, amefukuzwa jeshini na hawezi tena kupokea habari za kijasusi za jeshi.

Huwa ni kosa la jinai nchini Uholanzi kwa raia kusafiri ng'ambo kujiunga na IS.

Waholanzi takriban 180, wanaaminika kuondoka taifa hilo na kujiunga na makundi ya wapiganaji Iraq na Syria.

Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi, Jeanine Hennis Plasschaert, amesema litakuwa ni jambo la "kusikitisha" ikibainika kwamba mwanamume mmoja "ameungana na waovu" wenzake kwenye jeshi "wanahatarisha maisha kulinda haki na uhuru wa watu wengine."