Papa Francis ajipeleka kununua miwani

Papa Francis akijipima miwani Haki miliki ya picha AP
Image caption Papa Francis akiondoka dukani Roma baada ya kununua miwani

Papa Francis, alivutia umati mkubwa baada yake kufanya jambo lisilio la kawaida kwa kuondoka Vatican na kwenda dukani kujinunulia miwani.

Muuzaji miwani kwa kawaida huenda Vatican, na kuwasilisha miwani mipya lakini mara hii Papa Francis, alisisitiza kujipeleka kwenye duka hilo katikati mwa jiji la Roma.

Umati mkubwa ulikusanyika nje ya duka hilo ambalo alikaa karibu saa zima ndani, na mwisho akasisitiza ajilipie mwenyewe.

Papa aliandamana na msaidizi mmoja, mlinzi mmoja na maafisa kadha wa polisi kwenye safari yake hiyo.

Mtalii Mjerumani, Daniel Soehe, alisema alikuwa amekosa kumuona Papa Francis katika makao yake ya The Vatican mapema siku hiyo, lakini kwa bahati akamuona akiwa duka hilo la miwani.

"Nilimwambia babangu, 'Bwana we, hili hata lashinda kwenda St Peter's, kumuona Papa akiwa dukani akijipima miwani’,” aliambia shirika la habari la Associated Press.

Alipokuwa askofu mkuu wa Buenos Aires, alikuwa mara kwa mara akionekana akitumia magari ya usafiri wa umma au kutembea katika barabara za jiji.

Kwenye makala iliyochapishwa kwenye jarida la National Geographic la mwezi huu, Papa Francis amenukuliwa akisema: “Nimekuwa nikitaka sana mara nyingi kutembea katika barabara za jiji la Roma, kwa kuwa Buenos Aires nilipenda kutembea jijini.

“Nilifurahia sana kufanya hivyo. Kwa hili, najihisi kana kwamba nimefungiwa pahali.”