Ukarimu wa kupokea wahamiaji wapunguzwa

Kiongozi wa Austria, Werner Faymann (kushoto) Haki miliki ya picha AFP

Kiongozi wa Austria, Werner Faymann, amesema wakati umefika kuanza kupunguza hatua za dharura zilizochukuliwa, ambazo ziliruhusu maelfu ya wakimbizi kusafiri bila ya pingamizi kutoka Hungary, hadi Austria na Ujerumani.

Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani piya imeonya kwamba moyo mkunjufu wa kusaidia usiendekezwe.

Ilisema sheria za kutaka maombi ya hifadhi yashughulikiwe katika nchi ambapo wakimbizi wanawasili, bado zingaliko.

Na Juampili mchana, msafara wa magari kama 150 yakiendeshwa na wanaharakati wa Austria, ulivuka mpaka wa Hungary kwenda kuwachukua wakimbizi zaidi.

Msemaji wa polisi wa Hungary aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba wakuu wa Austria wamefahamisha wazi, kwamba mtu yoyote anayefanya hivyo, anavunja sheria.

Na Papa Francis amewaomba Wakatoliki Ulaya nzima kujitolea wawezavyo kusaidia kutatua msusuko wa wahamiaji.

Amependekeza kuwa kila parokia na jamii Ulaya inafaa kukaribisha familia ya wahamiaji.

Alisema parokia mbili za Vatikani zitaongoza kwa kukaribisha familia mbili.