Nigeria yapambana na ufisadi serikalini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hatua ya akaunti moja inalenga kupambana na vitendo vya udanganyifu

Muda uliotolewa kwa wizara za Serikali ya Nigeria kuhakikisha kuwa michakato ya huduma za kibenki zinafanyika kupitia akaunti moja ya Benki umefikia tamati.

Hatua hiyo imefikiwa ili kurahisisha ufuatiliaji wa mienendo ya matumizi ya Serikali ili kupambana na vitendo vya rushwa.

Akaunti hiyo itaratibiwa na Benki kuu ya nchini humo na inakadiriwa kuwa Benki za biashara zitapoteza kiasi cha dola bilioni kumi pesa zitakapohamishwa.

Wizara zitazoshindwa kutimiza agizo hilo zitawekewa vikwazo.

Rais Muhamadu Buhari, aliyetoa agizo la kufunga akaunti mbalimbali za benki amesema anaamini maafisa wa serikali wameiba kiasi cha dola bilioni 150 kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Naibu Gavana wa Benki kuu ya Nigeria,Obadiah Mailafia ameiambia BBC kuwa ilikuwa rahisi udanganyifu kufanyika kwa sababu Serikali haikujua kila wizara ina akaunti ngapi za benki.

Mwandishi wa BBC jijini Abuja amesema utekelezaji wa hatua ya ''akaunti moja'' umewezesha jimbo la kaduna kubaini kiasi cha dola milioni 13 ambazo awali zilikuwa hazifahamiki kama zilikuwepo.