Wakenya wapigania waziri kwenye Twitter

Anne Waiguru Haki miliki ya picha WAIGURU TWITTER
Image caption Waziri Waiguru amejitetea akisema ndiye aliyefichua kashfa ufisadi wizara yake

Waziri wa ugatuzi Kenya Anne Waiguru kwa siku kadha sasa amekuwa mada ya jumbe kwenye mitandao ya kijamii nchini humo na hasa Twitter, wengi wakitaka Rais Uhuru Kenyatta amsimamishe kazi.

Ni nini sababu ya kuvuma kwa jina lake mtandaoni? Yote yalianza kutokana na tangazo lake Ijumaa kwamba amewasilisha majina ya maafisa 21 wakuu kutoka wizara yake na Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa wachukuliwe hatua.

Hii ni baada ya afisi ya uchunguzi wa jinai kupendekeza washtakiwe kwa tuhuma za kula njama ya kulaghai NYS.

Bi Waiguru alisema uchunguzi umebaini Sh791 milioni zilitoweka kutoka kwa shirika hilo kupitia malipo ya kutiliwa shaka kwa kampuni za kibinafsi.

Wapinzani wa serikali ya Rais Kenyatta walichukua nafasi hiyo kukosoa juhudi zake za kupambana na ufisadi na kumtuhumu kumpendelea waziri huyo.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika mkutano wa kisiasa mtaa wa Kibera, Nairobi Jumapili alisema ndiye aliyekuwa wa kwanza kufichua kuhusu kashfa hiyo, na tangazo la Bi Waiguru lilionyesha kwamba alikuwa sahihi na kudai waziri huyo anakingwa na Rais Kenyatta.

Wakenya kwenye Twitter wamekuwa wakitumia vitambulishi mbalimbali kumtaka Bi Waiguru kujiuzulu, baadhi vikiwa #WhyWaiguruMustGo na #SuspendWaiguru.

"Ili kushinda vita dhidi ya ufisadi, hatufai kupendelea,” mmoja aliandika. "Huwezi kuruhusu wadogo wako waibe pesa kisha udai huna hatia. Lazima kuna pesa zilifika karibu naye,” aliandika mwingine.

Wanaomuunga mkono pia hawajaachwa nyuma, wakitumia vitambulisho vivyo hivyo kumtetea.

"Ufasaha, utendakazi mwema na ujasiri ni baadhi ya sababu ambazo zitamfanya Waiguru asiende popote,” mmoja wao aliandika. "Yeye ni mzalendo kamili na kiongozi mwanamke. Lazima tumuunge mkono,” ameongeza mwingine.