Wanyama waliohamia Kenya warudi Somalia

Simba Haki miliki ya picha Getty
Image caption Simba ni miongoni mwa wanyama ambao wameanza kuonekana tena Somalia

Baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Somalia, wanyama wa porini walitoweka na ilikuwa nadra sana kuwaona.

Wanamazingira wanasema kuwa kuna uwezekano wanyama hao waliuawa au wakatorokea katika nchi jirani ya Kenya.

Lakini sasa wanyama hao wameanza kuonekana katika maeneo ya Somalia, hasa yaliyo karibu na mpakani.

Wakazi wanasema wameona wanyama pori tofauti wakiwemo simba, twiga na ndovu na wanasema wanaamini kuwa wanyama hao ”wanarudi nyumbani”.

Operesheni ya kufurusha wanamgambo wa al-Shabaab msitu wa Boni, Kenya inadaiwa kuwa moja ya sababu zilizochangia wanyama hao kurejea Somalia kwani wanajihisi hawako salama huko.

Kamishna wa awali wa mji wa Badhadhe, Farah Haybe, ambaye ameishi katika mji huo kwa muda mrefu anasema kuwa wanyama hao wanakaribishwa.

”Tulikua tukiona wanyama kama hawa zamani na sasa hivi wanavuka mpaka. Wanarudi kutoka Kenya na tunawakaribisha.Tumewawekea walinzi wa usalama na itatubidi tukague vichinjio ili kuhakikisha hawachinjwi,” amesema.

Wanamazingira wanadai kuwa kutokana na kupungua kwa milio ya risasi katika sehemu nyingi za Somalia, hali imekuwa bora kwa wanyama pori.