Rais aliyepinduliwa Burkina Faso ‘huru’

Michel Kafando Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kafando alizuiliwa wanajeshi walinzi wa rais walipovamia mkutano wa baraza la mawaziri

Rais wa mpito wa Burkina Faso Michel Kafando aliyeondolewa mamlakani na kikosi cha walinzi wa rais ameachiliwa huru na yuko buheri wa afya, viongozi wa mapinduzi wamesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Isaac Zida, aliyezuiliwa wakati mmoja na walinzi hao walipovamia mkutano wa baraza la mawaziri, amewekwa kwenye kizuizi cha nyumbani.

Viongozi hao wa mapinduzi wamekubaliana kuhusu mambo muhimu ya kujadiliwa, huku marais wawili wa mataifa ya Afrika Magharibi wakiwasili nchini humo kuongoza mashauriano.

Rais Macky Sall wa Senegal na Thomas Boni Yayi wa Benin, walielekea Burkina Faso kufanya mashauriano na viongozi waliopindua serikali.

Haki miliki ya picha
Image caption Sall alipakia mtandaoni picha iliyomuonyesha akiwa kwenye ndege safarini kuelekea Burkina Faso

Rafiki wa karibu wa kiongozi wa zamani Blaise Compaore anayeishi uhamishoni Ivory Coast, Jenerali Gilbert Diendere, alitangazwa kiongozi mpya na walinzi hao Alhamisi.

Viongozi wa Amerika, Ufaransa na Muungano wa Afrika (AU) wameshutumu mapinduzi hayo.

Watu watatu wanadaiwa kuuawa baada ya wanajeshi wa kikosi hicho cha walinzi maalum wa rais (RSP) kuwakabili waandamanaji katika jiji kuu la Ouagadougou.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu wamekuwa wakiandamana Ouagadougou kupinga mapinduzi hayo

Shirika la kijamii lenye ushawishi mkubwa la Balai Citoyen limesema waliouawa ni 10.

Idadi isiyojulikana ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi hayo pia wamekamatwa na kuzuiliwa.

Viongozi hao wa mapinduzi wametangaza amri ya kutotoka nje usiku nchini humo na kufunga mipaka yote ya taifa hilo.