Diendere akwamilia mamlaka Burkina Faso

Gilbert Diendere Haki miliki ya picha
Image caption Jenerali Diendere anataka kuongoza hadi uchaguzi ufanyike

Jenerali aliyeongoza mapinduzi ya serikali Burkina Faso wiki iliyopita anataka kuendelea kuongoza taifa hilo hadi uchaguzi ufanyike, kwa mujibu wa mapendekezo yake ambayo BBC imefanikiwa kuyatazama.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa na Jenerali Gilbert Diendere kwa wapatanishi kutoka nchi za Afrika Magharibi, Rais Macky Sall wa Senegal na Rais wa Benin Yayi Boni, katika mji mkuu wa Ouagadougou.

Mnamo Jumamosi, Bw Boni alikuwa amezungumzia kupatikana kwa mafanikio na kudokeza kwamba kaimu rais Michel Kafando angerejeshewa mamlaka.

Watu zaidi ya 10 wameuawa kwenye makabiliano tangu kutokea kwa mapinduzi hayo Alhamisi.

Mapinduzi hayo ya serikali yaliyotekelezwa na kikosi cha walinzi wa rais yameshutumiwa vikali, na Burkina Faso imefukuzwa kutoka kwa Muungano wa Afrika.

Mwandishi wa BBC Afrika Magharibi Thomas Fessy amesema mapendekezo ya viongozi hao wa mapinduzi hayakusudii kurejesha mamlaka kwa utawala wa kiraia.

Mapendekezo hayo, yaliyotiwa saini na Jenerali Diendere na ambayo BBC imeyaona, yanasema anafaa kusalia uongozini hadi uchaguzi, ambao ulikuwa umepangiwa kufanyika Oktoba 11, ufanyike.

Hili ni tofauti sana na matumaini yaliyoelezwa Jumamosi na mmoja wa wapatanishi hao, Rais wa Benin Yayi Boni, aliyedokeza kwamba huenda walinzi hao wa rais wakakubali kuondoka mamlakani, mwandishi wetu anasema.

Jenerali Diendere alikuwa mkuu wa jeshi wa rais wa zamani Blaise Compaore, aliyetimuliwa madarakani kupitia maandamano Oktoba mwaka jana.

Wapatanishi wanatumai wataweza kumrejesha mamlakani Rais Michel Kafando

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hali ya wasiwasi bado inaendelea mji mkuu wa Ouagadougou

Hayo yakijiri, ghasia zilizuka Jumapili katika hoteli iliyoko Ouagadougou, ambako mazungumzo yamekuwa yakifanyika.

Kundi la watu 50 wanaounga mkono mapinduzi hayo liliingia ukumbi wa hoteli ya Laico, na kujeruhi watu kadha.

Nje ya jingo hilo, wapinzani wa mapinduzi hayo waliandamana lakini baadaye wakatawanywa na vikosi vya usalama.

Bw Kafando, ambaye awali alizuiliwa na viongozi hao, aliachiliwa huru. Hata hivyo, hatima ya Waziri Mkuu Isaac Zida, aliyezuiliwa wakati mmoja na rais huyo, bado haijabainika.