Watu 54 wauawa katika milipuko Nigeria

Majeruhi Maiduguri Haki miliki ya picha AP
Image caption Wapiganaji wa Boko Haram wamekuwa wakitekeleza mashambulio ya mara kwa mara Nigeria

Watu zaidi ya 54 wameuawa kwenye milipuko mitatu ya mabomu katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Msemaji wa jeshi la nchi hiyo amesema kundi la Kiislamu la Boko Haram, lililoasisiwa Maiduguri, lilihusika.

Polisi wameambia shirika la habari la Reuters watu 90 walijeruhiwa kwenye mashambulio hayo.

Mwandishi wa BBC Will Ross anasema sasa ni wazi kwamba mashambulio hayo ni mojawapo ya mashambulio mabaya zaidi kutekelezwa miezi ya hivi karibuni.

Bomu moja lililipuka katika msikiti, na mengine mawili yakalipuka eneo ambalo watu hukusanyika kutazama mechi za kandanda, msemaji wa shirika la kutoa huduma za dharura Muhammad Kanar amesema.

Milipuko hiyo Maiduguri inaashiria “kiwango cha juu cha kutamauka” katika Boko Haram, msemaji wa jeshi Sani Usman alisema kupitia taarifa.

Kundi hilo limekuwa likitaka kutekeleza uongozi wa Kiislamu kwa kutumia sharia maeneo ya kaskazini mashariki.

Watu milioni mbili wamefurushwa makwao tangu wapiganaji hao waanze harakati zao 2009.