Shule za kibinafsi zapata afueni Kenya

Shule ya Nyali
Image caption Baadhi ya shule ya kibinafsi ziliendelea na masomo kama kawaida

Shule za kibinafsi nchini Kenya zimepata afueni baada ya mahakama kusimamisha agizo la serikali la kutaka zifungwe pamoja na zile za umma kutokana na mgomo wa walimu.

Mahakama Kuu imetoa agizo hilo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Chama cha Shule za Kibinafsi kupinga agizo la wizara ya elimu lililotolewa Ijumaa.

Serikali ilikuwa imeagiza wanafunzi wote wasalie leo Jumatatu isipokuwa wale wanaojiandaa kwa mitihani ya kitaifa. Lakini mahakama ilisitisha agizo hilo upande wa shule za kibinafsi kwa siku tatu kusubiri kusikizwa kwa kesi hiyo.

Wanafunzi wengi shule za umma wamelazimika kusalia nyumbani baada ya serikali kuagiza kufungwa kwa shule zote za umma na wale wanaosomea shule za bweni wamelazimika kurudi nyumbani.

Hata kabla ya chama hicho cha shule za kibinafsi kwenda kortini, kilikuwa kimehimiza shule hizo kukaidi agizo hilo la serikali na baadhi ya shule hizo ziliendelea na masomo kama kawaida leo.

Mwandishi wa BBC Ferdinard Omondi alitembelea moja ya shule hizi mjini Mombasa. Mwalimu mkuu wa shule ya Nyali John Kombo alisema hakuona msingi wowote kisheria wa kuunga mkono agizo lililotolewa na Waziri wa Elimu Prof Jacob Kaimenyi.

Aidha, alisema walimu wa shule hiyo wanashughulikiwa ipasavyo na hilo liliwafanya kuendelea na kazi kama kawaida.

Hata hivyo alieleza wasiwasi kuhusu mitihani ya kitaifa akisema huenda ikaathiriwa na mgomo wa walimu ulioingia wiki ya nne leo.

"Tukiruhusu mgomo huu uendelee, tutaishia kuwa na watoto ambao wanamaliza shule bila kupata elimu wanayostahili kupata na hivyo watakuwa dhaifu kazini. Isitoshe, mitihani kama vile ya kemia inahitaji walimu kuiandaa vyema. Tunaomba mgomo huu usiendelee kwa muda mrefu," aliambia BBC.

Image caption Kombo ana wasiwasi kuhusu maandalizi ya mitihani ya kitaifa

Kwa mujibu wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) kuna watahiniwa 937,467 wanaojiandaa kufanya mtihani wa darasa la nane KCPE utakaoanza Novemba 10 na kumalizika Novemba 12.

Watahiniwa wanaojiandaa kufanya mtihani wa kidato cha nne KCSE utakaoanza rasmi Oktoba 12 ni 525,802.

Baraza hilo limesema mitihani hiyo haitaahirishwa.

Kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga, Rais Uhuru Kenyatta na baadaye kutumwa kwa vyombo vya habari alisema haiwezekani kwa walimu kuongezewa mishahara na kuwataka warejee kazini.

Mahakama ya Juu Kenya iliitaka serikali kutii agizo la mahakama ya rufaa iliyoitaka serikali kutii uamuzi wa mahakama ya kiviwanda na kuwalipa walimu nyongeza ya asilimia 50 hadi 60.

Serikali kupitia Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) imepinga agizo hilo.

Mahakama ya Viwanda inatarajiwa kutoa uamuzi Ijumaa wiki hii kuhusu iwapo mgomo huo wa walimu, uliotatiza masomo Kenya tangu zifunguliwe kwa muhula wa tatu, ni halali au la.