Papa awasili Marekani apokewa na Obama

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Papa Francis akikaribishwa Marekani na Rais Barack Obama

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasili nchini Marekani katika siku ya kwanza ya ziara ya kihistoria nchini humo ambapo amelakiwa na Rais wa nchi hiyo Barack Obama.

Papa Francis aliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Andrew Air Force Base kutoka nchini Cuba.

Huku Marekani ikiwa na zaidi ya waumini wa Katoliki wapatao milioni sabini ziara hiyo ya papa inaoneka kuwa tukio kubwa nchini humo.

Kiongozi huyo wa kidini ambaye anaitembelea Marekani kwa mara ya kwanza atafanya ziara na kuongoza ibada katika miji ya Washington, New York na Philadelphia.

Wakati Papa Francis akiondoka nchini Cuba Papa Francis aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye sio muumini wa mlengo wa kushoto kama wengi wanavyodhani.

Papa alisema hatazungumzia suala la vikwazo vya biashara kati ya Cuba na Marekani, licha ya kuchukua nafasi muhimu katika mazungumzo ambayo yamesababisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili kurejeshwa mapema mwaka huu.