Mahakama yasitisha mgomo wa walimu Kenya

Sossion
Image caption Wakuu wa chama cha walimu wameahidi kutoa taarifa baadaye

Mahakama nchini Kenya imesimamisha mgomo wa walimu uliodumu kwa wiki nne na kuwaagiza walimu kurudi kazini mara moja.

Jaji Nelson Abuodha wa mahakama ya kiviwanda na masuala ya wafanyakazi amesimamisha mgomo huo kwa miezi mitatu na kuwataka walimu na serikali kuunda kamati ya kutafuta suluhu katika muda wa mwezi mmoja.

Aidha, ameiagiza Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kutowaadhibu walimu na kuwalipa mishahara yao kikamilifu, pamoja na marupurupu. Tume hiyo ilikuwa awali imetishia kutowalipa walimu “kwa siku ambazo wamesusia kazi”.

Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo katika kesi iliyokuwa imewasilishwa na TSC kutaka mgomo wa walimu uliosababisha kufungwa kwa shule zote za umma kutangazwa kuwa “usiolindwa kisheria”.

Jaji Abuodha alisema mahakama inaweza tu kuamua kuhusu uhalali wa mgomo na akasema pia kuwa wafanyakazi wana haki kugoma.

Maafisa wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), moja ya vyama vilivyokuwa vimeitisha mgomo huo, hawajazungumza na wanahabari baada ya uamuzi huo lakini wameahidi kutoa taarifa.

Walimu waligoma wakitaka kulipwa nyongeza ya mishahara ya asilimia 50 hadi 60 ambayo mahakama ilikuwa imeagiza walipwe.

Wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alisema serikali haiwezi kulipa nyongeza hiyo.

Mgomo huo ulikuwa umetishia kuvuruga mitihani ya kitaifa inayotarajiwa kuanza hivi karibuni. Serikali wiki iliyopita ilikuwa imeagiza shule zote za umma zifungwe kuanzia Jumatatu wiki hii.

Kwa mujibu wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) kuna watahiniwa 937,467 wanaojiandaa kufanya mtihani wa darasa la nane KCPE utakaoanza Novemba 10 na kumalizika Novemba 12.

Watahiniwa wanaojiandaa kufanya mtihani wa kidato cha nne KCSE utakaoanza rasmi Oktoba 12 ni 525,802.