UN yatetea meli iliyozuiliwa Mombasa

Meli ya UN Haki miliki ya picha AP
Image caption Umoja wa Mataifa umesema silaha hizo zilikuwa zikisafirishwa kupelekwa DR Congo

Wiki moja baada ya vikosi vya usalama kuzuilia meli moja kutoka Norway katika bandari ya Mombasa, Umoja wa Mataifa umepuuzilia mbali madai kwamba silaha zilizopatikana ndani ya meli hiyo zilikuwa haramu.

Taarifa kutoka ofisi za UN jijini Nairobi imesemasilaha hizo, zilizokuwa zimewekwa ndani ya magari ya kijeshi, zilikuwa sehemu ya silaha halali zilizokuwa zikisafirishwa hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na zilipakiwa mjini Mumbai, India.

Aidha taarifa hiyo inaeleza kuwa ingawa silaha hizo hazikuwemo kwenye orodha rasmi ya mizigo ya meli hiyo, zilinakiliwa kwenye hati tofauti iliyonakili magari hayo.

UN imesema maafisa wa polisi Kenya walikiuka itifaki kwa kukagua meli hiyo bila kuwepo maafisa wa umoja huo.

Umoja huo umesema ni kawaida kwa silaha kama hizo kutengwa na kuwekwa ndani ya makontena ili zisiharibike zikisafirishwa.

Kadhalika, UN imesema inafahamu kuwepo kwa madai kwamba dawa za kulevya zilipatikana kwenye meli hiyo lakini ukaongeza kwamba suala hilo bado linachunguzwa.