Walinzi wa rais wakataa kusalimu silaha B Faso

Image caption Jenerali Diendere

Juhudi za kukipokonya silaha kikosi cha walinzi wa rais wa Burkina Faso kilichosalimu mamlaka wiki iliopita baada ya kufanya mapinduzi zimekwama kulingana na mkuu wa majeshi nchini humo.

Kiongozi wa mapinduzi hayo jenerali Gilbert Diendere amechukua msimamo wenye utata kuhusu hatua hiyo alisema jenerali Pingrenoma Zagre katika taarifa.

Kikosi cha walinzi wa rais kinashirikisha wanajeshi 1200.Viongozi wa Magharibi mwa Afrika waliafikia makubaliano ambayo yalitaka kikosi hicho kusalimu silaha zake na kurudisha mamlaka kwa serikali.

Siku mbili zilizopita mkuu huyo wa majeshi alikuwa amesema kuwa harakati ya kuwapokonya silaha wanajeshi hao ilikuwa inaendelea vyema.

Kaimu rais Michel Kafando alirudishwa mamlakani siku ya jumatano baada ya kundi linaloongozwa na jenerali Diendere kuwacha mamlaka kufutia shinikizo za kitaifa na kimataifa.