Wanajeshi Afghanistan wajaribu kukomboa Kunduz

Kunduz Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kutekwa kwa Kunduz ni changamoto kubwa kwa Rais Ashraf Ghani anayekamilisha mwaka mmoja mamlakani

Wanajeshi wa serikali nchini Afghanistan wanajaribu kuukomboa mji wa Kunduz, uliotekwa na wapiganaji wa Taliban Jumatatu.

Marekani imesema imeshambulia mji huo kutoka angani leo.

Wanajeshi wa Afghanistan walikuwa wametorokea uwanja wa ndege baada ya wapiganaji hao kuwazidi nguvu na kuachilia huru mamia ya wafungwa kutoka gerezani.

Shambulio hilo lilitokea huku Rais Ashraf Ghani akiadhimisha mwaka mmoja tangu kuingia mamlakani.

Hilo ndilo shambulio kubwa zaidi kutekelezwa na wapiganaji hao katika kipindi cha miaka kadha iliyopita na litamuongezea shinikizo Bw Ghani na serikali yake ya umoja.

Kunduz ndio mji mkuu wa kwanza wa mkoa kutekwa na Taliban tangu watimuliwe madarakani kupitia operesheni iliyoongozwa na Marekani 2001.

Mwandishi wa BBC Dawood Azami anasema changamoto kubwa sasa kwa wapiganaji hao jinsi watakavyoendelea kukwamilia mji huo.

Wanajeshi zaidi wameitwa kutoka mikoa iliyo karibu kujaribu kuukomboa.

Serikali imesema wapiganaji kadha wa Taliban na maafisa wawili wa polisi wameuawa kwenye mapigano.

"Mapigano makali yanaendelea,” afisa wa masuala ya ndani Matin Safraz aliambia shirika la habari la Reuters.

"Maafisa wa usalama wa Afghanistan wamekuwa wakikomboa maeneo muhimu ya mji huo na kuna ufyatulianaji wa risasi maeneo mengi,” amesema.

Mji wa Kunduz ni muhimu sana katika kufikia maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo.