Arsenal na Chelsea zaambulia patupu Uefa

Arsenal Haki miliki ya picha PA
Image caption Arsenal wanashika mkia kundi lao baada ya kushindwa mechi ya pili

Kilabu za Uingereza ziliendelea kuandikisha matokeo mabaya Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya baada ya Arsenal na Chelsea kucharazwa kwenye mechi zao Jumanne usiku.

Arsenal walijipata wakivuta mkia kundi F baada ya kupokezwa kichapo cha pili mfululizo na Olympiakos wakiwa kwao nyumbani.

Vijana hao wa Arsene Wenger walijiua walihitaji sana ushindi baada ya kushindwa na Dinamo Zagreb ya Croatia mechi yao ya kwanza, wakijua kwamba bado wanasubiri kucheza mechi mbili na Bayern Munich.

Badala yake walikubali kulala 3-2 uwanjani Emirates na sasa watakuwa wakipigania kuwa timu ya kwanza tangu Galatasaray msimu wa 2012-13 kushindwa mechi za kwanza mbili nab ado kufika hatua ya muondoano.

Mabao ya Arsenal yalifungwa na Theo Walcott na Alexis Sanchez nayo ya Olympiakos yakatokana na moja ya kujifunga la kipa wa Arsenal David Ospina, na mawili ya Felipe Pardo na Alfred Finnbogason.

Wengi wanashangaa ni kwa nini Wenger aliamua kumuweka langoni kipa Ospina badala ya Petr Cech.

Kwa Chelsea, mambo yaliwaendea mrama pia baada ya kushindwa 2-1 na Porto ya Ureno, ambayo iliwahi kunolewa na meneja wa sasa wa Chelsea Jose Mourinho.

Mabao ya Porto yalitoka kwa Andre Andre na Maicon, la kufutia machozi upande wa Chelsea likifungwa na Willian.

Mourinho alimuacha nje nyota wa msimu uliopita Eden Hazard, ilihali Radamel Falcao hakuwekwa hata kwenye benchi kwenye mechi hiyo iliyochezewa uwanja wa Estadio do Dragao.

Chelsea, walioanza vibaya msimu huu, watakuwa na mechi ngumu nyumbani dhidi ya Southampton Jumamosi, na wanatarajiwa kukutana na Dynamo Kiev mechi yao ya tatu Kundi G Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya Oktoba 20.