Watu tisa wauawa nchini Marekani

Haki miliki ya picha
Image caption Polisi wakiwa wamefunga barabara baada ya tukio la mauaji

Watu tisa wameuawa na wengine saba kujeruhiwa baada ya kutokea shambulio la risasi katika Chuo kimoja katika jimbo la Oregon, Polisi wameeleza.

Mtu mwenye silaha alifyatua risasi chuo cha Umpqua Alhamisi asubuhi na baadae kuuawa aipokuwa akijibizana kwa risasi na Polisi.

Kuna habari za kukanganya kuhusu madhara yaliyojitokeza lakini Afisa Polisi wa eneo hilo amesema Watu 10 wameuawa akiwemo muuaji huyo.

Polisi hawajamtambua muuaji lakini afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe ameviambia vyombo vya habari nchini Marekani kuwa jina lake ni Chris Harper Mercer.

Sababu za muuaji huyo kutekeleza shambulio hazijajulikana, ingawa Polisi wanasema wanafanyia uchunguzi ripoti kuwa alitahadharisha dhamira yake katika mtandao wa kijamii.

Saa kadhaa baada ya shambulio, ambalo watu saba walijeruhiwa Rais wa Marekani, Barack Obama ametaka kuwe na sheria kali za udhibiti wa silaha.