Rais Kikwete kuhutubia Bunge la Kenya

Jakaya Kikwete
Image caption Atakuwa kiongozi wa pili wa taifa la kigeni kuhutubia Bunge nchini Kenya

Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete atahutubia bunge la Kenya Jumanne wiki ijayo huku akiendelea kujiandaa kuondoka mamlakani.

Kiongozi huyo atahutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Bunge la Seneti katika majengo ya bunge jijini Nairobi.

Rais Kikwete atakuwa kiongozi wa pili wa taifa la nje kuhutubia bunge Kenya. Aliyekuwa kiongozi wa Nigeria Goodluck Jonathan alikuwa kiongozi wa kwanza kuhutubia bunge la Kenya Septemba 6, 2013.

Spika wa Bunge la Kitaifa Kenya Justin Muturi aliambia wabunge Alhamisi kwamba Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amemwandikia akiomba ruhusa kiongozi huyo mwenzake akubaliwe kuhutubu.

“Ningependa kuwajulisha kwamba, baada ya kufanya mashauriano, Spika wa Seneti nami tumekubali ombi hilo,” Bw Muturi aliambia wabunge.

Kwa muda sasa, Rais Kikwete amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali ya Tanzania akiwaaga wananchi.

Uchaguzi mkuu nchini Tanzania utafanyika Oktoba 25.

Bw Kikwete aidha hatakuwa kiongozi wa kwanza kuhutubia bunge la taifa jingine Afrika Mashariki.

Majuzi Agosti 10, 2015 Rais Kenyatta alihutubia bunge la Uganda wakati wa ziara rasmi ya siku tatu.