Mwanasiasa mashuhuri afariki Tanzania

Image caption Hayati Mchungaji Christopher Mtikila

Mwanasiasa mashuhuri na mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP)nchini Tanzania, Mchungaji Christopher Mtikila amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Chalinze mkoani Pwani.

Pamoja na shughuli za kisiasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa Kanisa la Kipentekoste la Full Salvation Church, wakati huo huo akijihusisha na harakati za haki za binadamu.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Mchungaji Mtikila alijipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja, upinzani wake dhidi ya muundo wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu uhujumu wa uchumi uliokuwa unafanywa na Wahindi (ambao aliwaita Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za Tanzania.

Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar huku akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na siyo Tanzania. Hata hivyo Mtikila alibadili msimamo wake katika miaka ya karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama kutoka Zanzibar hivyo chama chake kuweza kupata usajili wa kudumu.

Mwaka 2005, Mtikila alikuwa ni kati ya wagombea 10 wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu na kupata asilimia 0.27 ya kura zote.

Mwaka huu alishindwa kupata nafasi ya kuingia kwenye kinyanganyiro cha uraisi mara baada ya kuchelewa na kufika tume ya uchaguzi bila mgombea mwenza.

Alipata umaarufu mkubwa kwa kesi zake zilizokuwa zikiendelea ambapo hata leo alikua anategemea kusikiliza rufaa ya moja ya kesi zake inayohusiana na uhalali wake kugombea Urais..

Miongoni mwa Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja na kesi ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya na polisi.

Hata hivyo Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba.

Mwaka 2004 alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala, jijini Dar es salaam.